Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano
maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, Waamini walei, Wakleri na Watawa kwa pamoja
wanaunda Taifa la Mungu.
Mtaguso mkuu
wa Pili wa vatican unabainisha nafasi, utume, karama na mchango maalum wa waamini
walei katika maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni. Kuna majimbo ambayo yamepiga hatua
kubwa kwa waamini walei kuelewa wito na maisha yao ndani ya Kanisa na kwamba, wanajitahidi
kuuishi Ukristo wao kikamilifu.
Waamini walei wanaoishi kikamilifu Ukristo
wao wanatekeleza karama ya Pentekoste, siku ambayo Roho Mtakatifu alilishukia Kanisa
na kutia nguvu ya kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.
Ushuhuda wa waamini walei ni tunda la mshikamano wao wa ubatizo na Kristo mfufuka.
Wao ni watoto wa Pasaka na Penteskote.
Askofu mkuu Ruwaichi anasema kwamba,
Kanisa linapoajiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili
ya Familia, iwe ni fursa ya kuangalia pia mapungufu yanayojitokeza katika maisha ya
waamini walei kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa.
Wakleri wajichunguze na kuangalia pale ambapo wamekuwa ni kikwazo kwa ustawi na maendeleo
ya waamini walei ndani ya Kanisa, kiasi kwamba, wanashindwa kushiriki kikamilifu katika
mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, ili kurekebisha kasoro
hizi na kuanza kuwashirikisha waamini walei kikamilifu, kila upande ukitambua na kuheshimu
karama na dhamana yake ndani ya Kanisa.