Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 7 Juni 2014 amewapongeza vijana wanaofanya
hija ya 36 ya maisha ya kiroho kutoka Macerata kuelekea Loreto katika mkesha wa Siku
kuu ya Pentekoste na anataka kuwahakikishia uwepo wake wa kiroho katika tukio hili
muhimu katika maisha yao ya kiroho. Anawashukuru na kuwapongeza kwa kuendelea kuombea
amani huko Mashariki ya Kati, ili dunia iweze kusikia kwa mara nyingine tena ule wimbo
wa Malaika "Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema".
Baba
Mtakatifu ametuma ujumbe huu kwa njia ya simu na kuzungumza na vijana hawa moja kwa
moja kutoka mjini Vatican. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya ni "Mwenyezi Mungu
mwingi wa miujiza", jambo ambalo ni kweli, kumbe vijana hawana budi kushangaa, kuomba
na kumuuliza Mwenyezi Mungu ili kukuza na kudumisha zawadi ya imani ambayo wanakirimiwa
na Mwenyezi Mungu.
Hii ni zawadi ambayo wanapaswa kuiboresha kwa uvumilivu,
mafanikio na wakati mwinginie kwa shida na magumu, lakini hakuna sababu ya kuogopa
kwani Mwenyezi Mungu atawabariki na kuwakirimia kadiri ya mahitaji yao! Kamwe vijana
wasiwaogope wale wanaotaka kuwapokonya ndoto hii njema na badala yake, watoe kipaumbele
cha kwanza kwa mwanga wa matumaini, wakiwa na mwelekeo chanya wa maisha unaojikita
katika furaha wanayowashirikisha wengine.
Matumaini kamwe hayawezi kudanganya
na kwa Mungu hakuna kinachoweza kupotea, lakini bila Mungu yote ni ubatili mtupu!
Huu ni mwaliko kwa vijana kumfungulia Mungu malango ya mioyo yao, ili macho yao yaweze
kuona tena njia na matendo yake makuu!