Roho Mtakatifu anafundisha, anakumbusha, anasali na kufanya unabii!
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pentekoste, tarehe 8 Juni
2014 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa mahubiri yake anasema
kwamba, Yesu aliwaahidia Mitume wake zawadi kutoka kwa Baba, yaani Roho Mtakatifu
na ahadi hii inatekelezwa wakati wa Siku kuu ya Pentekoste.
Hili ni tukio
endelevu linaojionesha katika maisha na utume wa Kanisa, kwani Roho Mtakatifu analihuisha
Kanisa, anawafundisha, anawakumbusha na kuwasaidia waamini kuzungumza.
Papa
Francisko anasema, Roho Mtakatifu ni mwalimu wa maisha yandani anayewaonesha waamini
dira na njia ya maisha kama alivyofanya wakati wa Kanisa la mwanzo. Roho Mtakatifu
ni njia kama alivyo Yesu mwenyewe, kwani anawasaidia waamini kumfuasa Kristo na kutembea
katika nyayo zake. Roho Mtakatifu ni mwalimu wa maisha, ujuzi na maarifa katika uwepo
na utume wa maisha ya Kikristo.
Roho Mtakatifu anawakumbusha waamini yale ambayo
Yesu amewafundisha mitume wake, ni kumbukumbu hai ya Kanisa anayewakumbusha waamini
uwepo endelevu wa Kristo katika maisha na utume wa Kanisa. Ni Roho wa ukweli na upendo
anayedai jibu makini kutoka kwa waamini kwa njia ya maneno ya Yesu yaliyomwilishwa
katika ushuhuda wa maisha pamoja na kukumbushwa kuiishi ile amri kuu ya mapendo kwa
Mungu na jirani.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amewataka waamini kuzingatia
umuhimu wa historia ya Ukristo kwa kuisoma na kuimwilisha kama sehemu ya histoaria
ya ukombozi na kwamba, Roho Mtakatifu anawasaidia kuyaangalia yote haya katika mwanga
wa mafundisho ya Yesu na hivyo kukuza hekima moyoni ambayo kweli ni zawadi kutoka
kwa Mwenyezi Mungu.
Roho Mtakatifu anawajalia waamini kumbukumbu ya kuweza
kuzungumza na Mungu pamoja na wengine kwa njia ya sala kwa kutambua kwamba, wao ni
watoto wateule wa Mung. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kushiriki katika majadiliano
ya kidugu ili kujenga na kuimarisha urafiki, amani na utulivu kwa kutambua mateso
na matumaini; wasi wasi na furaha kwa wengine.
Roho Mtakatifu anawawezesha
waamini kuwa kweli ni Manabii wanyenyekevu wa Neno la Mungu, ili kukemea kinzani na
ukosefu wa haki, ili kuponya na kujenga kwa kutumia upendo, ili kweli waamini waweze
kuwa ni vyombo vya Mungu anayependa, anayehudumia na kugawa zawadi ya uhai.
Kwa
ufupi Baba Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu anawafundisha waamini njia ya maisha,
anawakumbusha na kuwafundisha Maneno ya Yesu; anawasaidia kusali na kumwita Mwenyezi
Mungu, Abba, yaani Baba; anawafundisha kujadiliana na wengine na kuonesha unabii.
Siku kuu ya Pentekoste ni siku ya Ubatizo wa Kanisa linalotumwa kuwatangazia
watu wote Habari Njema ya Wokovu. Mitume kwa kupokea nguvu ya Roho Mtakatifu wanaanza
kutekeleza utume wao wa Kuinjilishaji kwani bila Kristo hakuna Uinjilishaji, ndiyo
maana Kanisa linamwita na kumwomba Roho Mtakatifu!