2014-06-08 08:54:44

Ninyi ni mashahidi wa Kristo Mfufuka!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anawapongeza askari wote wa vyombo vya ulinzi na usalama wanaotoa huduma mjini Vatican kwa kazi kubwa na nzuri wanaoitekeleza katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza kwa weledi, majitoleo, dhamana na uwajibikaji wao katika masuala ya ulinzi na usalama mjini Vatican na kwa ajili ya wote wanaofika Roma kufanya hija kwenye makaburi ya watakatifu Petro na Paulo bila kuwasahau wanaofika kumsikiliza Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kardinali Parolin ameyasema hayo Jumamosi, tarehe 7 Juni 2014 wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya askari wa vyombo vya ulinzi na usalama wanaotekeleza majukumu yao mjini Vatican. Hii ni huduma inayotekelezwa kwa hali ya unyenyekevu na majitoleo makuu; katika utulivu na huduma kwa Jamii. Vatican ni mji ambao una utajiri mkubwa wa sanaa, lakini umesheheni idadi kubwa ya mahujaji wanaofika kusali na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hapa ni kivutio kikuu cha watalii kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Vatican ni makao makuu ya Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume!

Huduma inayotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama inawawezesha watu kuonja amani na utulivu mioyoni mwao, kiasi cha kuendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya zawadi ya imani kwa Yesu Kristo Mnazareti. Kanisa linaendelea kumshukuru Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, changamoto kwa waamini kuendelea kuwa waaminifu kwa kuonesha upendo wa dhati kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kumtegemea Roho Mtakatifu anayeliongoza Kanisa katika maisha na utume wake.

Kardinali Pietro Parolin anawataka waamini kujenga moyo wa ibada, heshima na kuaminiana kila mtu akitekeleza dhamana na wajibu wake katika maisha na utume wa Kanisa, wakiongozwa na upendo kwa Mungu na jirani. Kila mwamini ajitahidi kuwa ni shahidi na mtangazaji wa Yesu Kristo Mfufuka mintarafu huduma anayoitoa mbele ya jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.