Mara baada ya maadhimisho ya Ekaristi Takatifu katika Sherehe ya Pentekoste, Jumapili
tarehe 8 Juni 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Wakati
wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Baba Mtakatifu anasema kwamba, Pentekoste inafunga kipindi
cha Pasaka kwa mshangao mkubwa, kwa Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume, kiasi kwamba,
wanapata ujasiri na nguvu ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayoeleweka na wote!
Mahali ambapo Roho Mtakatifu anafika, kunabadilika na huu ndio mwanzo wa Kanisa linalojidhihirisha
hadharani, ni Kanisa linaloshangaza na kuonesha "vurugu".
Pentekoste anasema
Baba Mtakatifu ni Sherehe ya kushangaza, kwani hakuna mtu aliyekuwa anategemea jambo
lolote kutoka kwa mitume baada ya kifo cha Kristo, ni watu waliobaki kama watoto yatima,
Pentekoste inawashangaza wengi kwani kila mtu aliweza kusikia Habari Njema ikitangazwa
kwa lugha yake mwenyewe, matendo makuu ya Mungu.
Kanisa lililozaliwa wakati
wa Pentekoste linazua mshangao kwani linaanzishwa kwa nguvu ya Mungu na kutangaza
Ufufuko wa Kristo kwa lugha ya upendo. Mitume wamejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu na
wanazungumza kwa ujasiri na ukweli kadiri ya Roho Mtakatifu. Hivi ndivyo Kanisa linavyopaswa
kuwa na nguvu ya kutangaza Kristo aliyeshinda kifo na kwamba, Mwenyezi Mungu kwa njia
ya uvumilivu yuko tayari kuwaponya na kuwasamehe, utume ambao Yesu amelikabidhi Kanisa
lake.
Baadhi ya watu mjini Yerusalemu walitaka kuwaona mitume wa Yesu wakiwa
wamejifungia ndani bila kusababisha vurugu kama zile zilizojitokeza wakati wa Pentekoste,
lakini Yesu anawatuma ulimwenguni kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Hili ni Kanisa
ambalo liko kwa sababu linatumwa kukutana na watu ili kuwatangazia Habari Njema ya
Wokovu hata kama Habari hii itahangaisha dhamiri za watu. Ni Kanisa linalokumbatia
ulimwengu bila kumezwa.
Bikira Maria alikuwepo siku ile ya Pentekoste akiwa
anasali na Mitume wa yesu. Ndani mwake, Roho Mtakatifu ametenda mambo makuu, kwa kumwezesha
kuwa ni Mama wa Mkombozi na Mama wa Kanisa.
Mara baada ya Sala ya Malkia wa
Mbingu, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema
wanaoungana nao, yaani Papa Francisko, Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Marais kutoka
Israeli na Palestina kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati.