Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 7 Juni 2014 ameshiriki katika maadhimisho
ya miaka 70 ya Chama cha Michezo Italia CONI kwa kukutana na kuzungumza na umati wa
vijana waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro pamoja
na viunga vyake.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, anatambua umuhimu wa michezo
kama mang'amuzi ya malezi, jambo linalowahusisha wadau wote wa michezo. Hii ni njia
muhimu sana katika malezi na majiundo ya watoto na vijana, katika mwelekeo wa kujitafutia
kazi, kujitegemea na kuwa makini katika maadili na utu wema, bila kuwa "mateja" wa
dawa za kulevya wala ulevi wa kupindukia.
Shule, michezo na kazi ni mambo
muhimu sana katika maisha ya ujana kwa ajili ya afya ya roho na mwili. Michezo iwasaidie
vijana kutafuta mafao ya wengi ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake; michezo
iwawezeshe vijana kukutana na Mwenyezi Mungu ili kupata taji lisiloharibika kamwe!
Michezo ni shule ya ukarimu inayowajengea watu huweza wa kuwafungulia wengine milango
ya maisha yao, lakini zaidi kwa wale ambao hawakubahatika katika jamii, ili nao waweze
kushirikisha karama na vipaji vyao!
Michezo ni dhamana inayowajibisha na kuchosha,
lakini inamwezesha mchezaji kupata haki, uzuri na kushirikiana na wengine ili kuondokana
na upweke hasi, ubinafsi na uchoyo katika maisha. Michezo ni fursa ya kukutana na
kusaidiana katika maisha, kwa kuheshimiana na kukua pamoja kama ndugu. Ni mahali pa
kukuza na kuimarisha miito mitakatifu ya maisha ya kipadre na kitawa, ndiyo maana
michezo Parokiani ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha pekee kadiri ya maisha
na utume wa Kanisa. Michezo ni chachu ya umissionari ndani ya Kanisa, inayowawezesha
watu kukutana na Yesu Kristo!
Baba Mtakatifu anawashukuru wanamichezo kwa kumteuwa
kuwa ni Kapteni wao, changamoto ya kushikamana ili kujenga na kuimarisha umoja kama
timu na kwamba, mchezo mkubwa ulioko mbele yao ni kutangaza Injili ya Furaha kwa watu
wa mataifa. Kila mwanamichezo ashirikishe kipaji na karama yake kama alivyohimiza
Yesu kwa wafuasi wake, ili kuwashirikisha wengine matumaini na imani. Kwa wanamichezo
wanaojikita katika shule, kazi na michezo, kwani matumizi haramu ya dawa za kulevya
au ulevi wa kupindukia hauna nafasi kamwe.
Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia
kheri na baraka katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pentekoste na amewaomba wazidi kumwombea
ili aendelee kutekeleza dhamana na wajibu wake kadiri ya mapenzi ya Mungu hadi pale
Mwenyezi Mungu atakapomwita kwenye makao ya uzima wa milele.
Siku hii imefunikwa
kwa michezo mbali mbali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
mjini Vatican pamoja na viunga vyake. Wanamichezo walipata fursa ya kushiriki pia
Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Italia