Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pentekoste linasema
kwamba, vyama mbali mbali vya kitume vinavyotekeleza dhamana yake ndani ya Kanisa
Katoliki ni alama na kielelezo cha nguvu ya Roho Mtakatifu katika ulimwengu mamboleo.
Kila mwanachama wa chama na mashirika ya kazi za kitume anapaswa kutolea ushuhuda
wa imani yake kwa njia ya matendo kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.
Imani hii tendaji inaweza kutekelezwa hata katika hali ya ukimya pasi na makeke, lakini
inakuwa ni chachu katika kuyatakatifuza malimwengu, ili dunia iweze kuwa ni mahali
pazuri zaidi pa kuishi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linakazia kwa namna
ya pekee kabisa neema ya kushikamana ili kujenga umoja na udugu, waamini wote wakitambuana
kuwa ni kaka na dada katika Kristo, kwani Roho Mtakatifu anawaongoza wote kuelekea
katika umoja na mshikamano katika mambo matakatifu. Roho Mtakatifu ni mdau mkuu wa
Uinjilishaji, changamoto ya kujitosa kimasomaso kuwaendea maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii kutokana na utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Vyama na mashirika ya kitume yajipambanue kwa kutafuta uzuri, ukweli pamoja
na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Karam ana mapaji ya Roho Mtakatifu
yatumike kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na Jamii inayowazunguka. Ni wajibu
wa kila chama na shirika la kitume kupyaisha na kumwilisha karama yake katika uhalisia
wa maisha ya watu wanaowazunguka, ili kweli Injili ya Furaha iweze kuwagusa na kufahamika
na watu wengi zaidi!