2014-06-07 07:13:06

Ujumbe wa Pentekoste kutoka Halmashauri ya Walei Tanzania


Neema na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alijitoa Nafsi yake kwa ajili yetu na kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na Uovu wa dunia; hii ya sasa, Utukufu una yeye sasa na milele yote Amina.


Yesu alipokutana na wafuasi wake kabla ya kupaa mbinguni aliagiza wasitoke Yerusalemu hadi waipokee ahadi ya Baba ambayo aliwaambia habari zake “Yohana alibatiza kwa maji lakini ninyi,mtabatizwa kwa Roho mtakatifu baada ya siku hizi chache(Mdo 1:5).”Yesu aliendelea kusema “Mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu, Roho mtakatifu nanyi mtakuwa mashahidi wangu, katika Yerusalemu na katika Uyahudi yote na Samaria na hata mwisho wa nchi (Mdo 1:8)”.


Hii ina maana Roho Mtakatifu ni mwezeshaji mkuu na usipojazwa na Roho Mtakatifu (Pentekoste mpya) hutaweza kumshuhudia Kristo wala Neno la Mungu halitakaa ndani mwetu. Roho Mtakatifu ni nguvu ya Yesu ndani mwetu.

Tutapokeaje Pentekoste mpya , yaani Roho Mtakatifu?

Hatuwezi kupokea Pentekoste mpya yaani Roho mtakatifu hadi tumwamini Yesu na kukaa katika neno lake hadi tuwe wanafunzi wake kweli-kweli. Kuwa wanafunzi wake kweli-kweli maana yake ni kuwa wafuasi wake kimatendo.


Tusimwamini Yesu kama tunavyomwamini mganga wa kienyeji, lazima tuwe na uhusiano binafsi naye. Yesu mwenyewe ndiye anayempeleka Roho Mtakatifu hivyo lazima tulijue Neno lake na kulipa nafasi katika mioyo yetu; na kumruhusu yeye atawale maisha yetu kila siku. Hii inadai kufanya ”Metanoia” yaani toba ya ndani na endelevu na kuelekea maisha mapya kabisa.


Hapa Kanisa limeweka Sakramenti ya Kitubio ambayo ipo kila siku ili nasi tujitakase kila siku, tunapoanguka dhambini bila kufanya hivyo, tukiiishi katika dhambi Roho Mtakatifu anaondoka kwetu. Kulipa nafasi neno la Yesu ni lazima kwanza ulisome na ulisikilize ili kumfahamu Yesu na baadae umjue kwa kujifunza neno lake na kulifanya neno lake kuwa nyumbani kwetu na kukaa katika neno hilo. Tukilijua neno la Mungu tunafanyika kuwa waana, na mwana hukaa nyumbani kwa Baba yake. “Mtumwa hakai nyumbani siku zote lakini mwana hukaa nyumbani siku zote” (Yoh.8:35) “kutokufahamu maandiko ni kutokumfahamu Yesu wakati yeye ni njia kweli na uzima” Yoh 14:6).

Tukimpa nafasi Yesu moyoni mwetu atatupa Pentekoste mpya. usimwendee Yesu wakati wa shida tu,lakini wakati mwingine hatuna habari naye. “Wale wanaomfuata na kujifunza maisha yake huchukuwa msalaba na kwenda nyuma yake” (Mt 16:24-27). usidanganyike kwa Yesu ni tambarare, kama wanavyosema wengine. Kwa Yesu kuna hitaji bidii na uvumilivu pia kwani kuna milima na mabonde.


Pengine mara kwa mara tunakwenda Kanisani ili kutimiza wajibu tu na kama mazoea lakini hatumpi Yesu nafasi katika kufanya maamuzi yeyote katika maisha yetu. Imani ya namna hii si nzuri kwani hata shetani anahudhuria kanisani lakini si kwa sababu za kumwambudu Mungu: Yakobo anasema “wewe waaamini Mungu ni mmoja watenda vyema ,mashetani nao wanaamini na kutetemeka” (Yako 2:19). Mkristo anaye amini namna hii hata akiwa kiongozi hawezi kuwa mfuasi huru na mtendaji maana Roho wa Mungu afanyi kazi ndani mwake.


Lazima tumwamini Yesu na kukaa katika neno lake “Tusiunganishwe na kila wimbi la mafundisho na kupeperushwa kwa kila upepo wa elimu mpya” (Ebr. 4:14). Yesu anasema hivi “angalieni mtu asiwachanganye kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema mimi ni kristo nao watawadanganya wengi”. “Tazama Kristo yuko hapa au yuko kule, msisadiki kwa maana watatokea ‘Makristo’ wa uongo na manabii wa uongo nao watatoa ishara kubwa na maajabu wapate kuwapoteza kama yamkini hata waliowateule.Tazama nimekwisha kuwaonya mbele” (Mt.24:3-4; 23-25).


Lazima tujue neno la Mungu na hukubali kuwa wanafunzi wa Yesu maana yeye ndiye hasa mwalimu wa kweli, naye ndiye atakayekupa kipawa cha Roho mtakatifu.

Roho Mtakatifu ndiye atakayetufanya tutambue ukweli na kutuweka kwenye kweli yote (Yoh 16:12-13). Ukweli wa Kristo humweka mtu huru. Roho Mtakatifu hatakaa kwetu kama tutaendelea kuikumbatia dunia na mambo yake, kama vile uasherati, uzinzi, ulevi, uchawi, mila potofu, ufisadi, mizimu na mambo mengine yanayofanana na hayo. Wakristo wakatoliki tuinuke tuchuchumilia ufalme wa mbinguni ambako kuna raha ya kweli.


    Roho Mt. aliwawezesha wale wafuasi kuwa na ujasiri wa kusema ukweli, kuhubiri na kuongoza.
    Roho Mtakatifu aliwajenga katika umoja wa utendaji. Mitume wakawa watendaji bora, wenye kujituma, kushirikisha na kushauri. Walei wawezeshwaji na Roho Mtakatifu inawapasa kuishi na kutenda kama mitume katika mazingira na jamii yao.
    Roho Mtakatifu aliwajenga katika maisha ya uaminifu na majitoleo. Walei tuombe kujazwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu.
    Walei wale wa Kanisa la mwanzo wakiwezeshwa na Roho Mtakatifu walikuwa waponyaji wa watu kwa:

      Huduma ya upendo kwa wenye shida, wanyonge na wagonjwa.
      Ushauri kwa wenye matatizo
      Watetezi wa kweli wa wanajamii hususan masuala ya haki
      Maisha mema ya Imani ya kina na kweli, upendo na umoja.


Hii ni changamoto kwetu leo hii. Ndugu zangu tupo wapi katika mitazamo, utendaji na maisha ya Kikristo, yaani ya ukatoliki kweli kweli?


Gasper Makiluli
MWENYEKITI HALMASHAURI WALEI TAIFA








All the contents on this site are copyrighted ©.