2014-06-07 09:07:05

Shukrani kwa Rais Museven kwa ulinzi na usalama!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda limeishukuru Serikali ya Uganda kwa kuhakikisha ulinzi na usalama wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashahidi wa Uganda iliyofanyika hivi karibuni pamoja na kuwashukuru viongozi mbali mbali wa Serikali walioshiriki katika maadhimisho haya kielelezo cha umoja na mshikamano katika mambo msingi.

Hayo yamebainishwa na Padre Philip Odii, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda wakati wa mahojiano maalum na Gazeti la AMECEA linalochapisha habari zake kwenye mtandao. Serikali ilihakikisha kwamba, vyombo vya ulinzi na usalama vinatekeleza wajibu wake barabara ili kuwawezesha waamini kutoka ndani na nje ya Uganda kuadhimisha kumbu kumbu ya Mashahidi wa Uganda kwa amani na utulivu, kielelezo makini cha utekelezaji wa uhuru wa kuabudu, dhidi ya vitisho vya mashambulizi ya kigaidi ambavyo vimeendelea kuwajengea watu hofu kubwa katika siku za hivi karibuni.

Viongozi mbali mbali wa kidini na serikali wanaendelea kuwaonya wananchi wa Uganda kuwa makini dhidi ya watu wanaoweza kujipenyeza nchini humo na hivyo kusababisha vitendo vya kigaidi.

Ibada ya Misa Takatifu iliyongozwa na Askofu Giuseppe Filippi kutoka Jimbo Katoliki la Kotido, Uganda. Katika mahubiri yake, amewaonya waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutomezwa na malimwengu kwa kupenda mno mali na madaraka, mambo ambayo yamekuwa ni chanzo cha kupotea kwa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya Jamii nyingi Barani Afrika. Ikiwa kama Jamii itasimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, watu wataweza kuishi kwa amani na utulivu.

Askofu Giuseppe Filippi aliwataka watu waliobahatika kuwa na fedha pamoja na mali, kuonesha upendo na mshikamano na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Amewataka pia kupambana kufa na kupona na vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyokwamisha maendeleo ya watu na hivyo kusababisha kinzani na migogoro ya kijamii. Mashahidi wa Uganda walionesha moyo wa upendo na ukarimu kwa maskini na wahitaji, wakatoa mali yao kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa na kueneza Habari Njema ya Wokovu.

Rais Yoweri Kaguta Museven wa Uganda amewataka viongozi wa kidini nchini Uganda kujifunga kibwebwe kushiriki katika mapambano dhidi ya umaskini nchini Uganda kwa kuchangia kwa hali na mali sera, mipango na mikakati ya Serikali kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza kipato cha familia!







All the contents on this site are copyrighted ©.