2014-06-07 12:26:30

Sala ya kuombea amani Mashariki ya Kati!


Baba Mtakatifu Francisko anasema umefika wakati wa kubomoa kuta zinazowatenganisha watu na badala yake kujenga madaraja yanayowaunganisha watu na hivyo kujisikia kuwa ni ndugu wamoja hata katika tofauti zao za kimsingi. Umefika wakati wa kuondokana na falsafa ya kinzani na kichongo na badala yake kujenga amani, utulivu na umoja wa kweli!

Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2014 itakuwa na umuhimu wa pekee pale ambapo Baba Mtakatifu Francisko ataungana na Rais Shimon Peres wa Israel na Rais Mahamoud Abbas wa Palestina kumwomba Mungu wa amani aweze kuwajalia wananchi wanaoishi Mashariki ya Kati kupata amani ya kudumu. Sala hii inatarajiwa kufanyika kwenye Bustani za Vatican majira ya jioni.

Hii si sala ya majadiliano ya kidini, bali ni kipindi cha kukaa na kutafakari kwa pamoja wote wakimwelekea Mwenyezi Mungu kuomba amani kwa kutambua kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi mungu inayomwajibisha pia mwanadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa watu wa amani katika sala na matendo.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii anasema kwamba, sala inaweza yote! Anawaalika watu kusali kwa ajili ya kuombea amani Mashariki ya Kati pamoja na sehemu mbali mbali duniani.All the contents on this site are copyrighted ©.