2014-06-07 14:58:51

Roho Mtakatifu analitakatifuza Kanisa!


Uje Roho Mtakatifu, uzienee nyoyo za waamini wako.
Sala kwa Roho Mtakatifu; Peleka roho wako vitaumbwa vipya na nchi itageuka.

Tuombe:
Ee Mungu, uliyefundisha nyonyo za waamini ukiwaletea mwanga wa roho mtakatifu, tunaomba tuongozwe na yule roho, tupende yaliyo mema, tupate daima faraja zake. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu amina.

Mhubiri maarufu Padre Raniero Cantalamessa anatoa mfano huu; bila shaka kila mmoja au wengi wetu tumeshiriki kusukuma au kuona watu wakisukuma gari bovu. Wengine hukaa nyuma, wengine pembeni n.k isipowaka mara ya kwanza, husimama, hufuta jasho, hukusanya nguvu tena na halafu hatua ya pili inafuata. Likiwaka, wanaosukuma hufurahi, hushangilia na hata kupiga miluzi. Maisha yetu ya kikristo huenda hivyo, pengine kwa nguvu nyingi lakini bila maendeleo thabiti. Leo tunakumbushwa tena na injili ya kikristo juu ya nguvu kutoka juu inayodai lakini nafasi katika mioyo yetu.

Sherehe ya Pentekoste hutukumbusha tena nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu na hutupatia tena msukumo mpya wa kiimani.

KATIKA SALA YA NASADIKI:
    MUNGU BABA – ANAUMBA
    MUNGU MWANA AU KRISTO – ANAOKOA
    MUNGU ROHO MTAKATIFU – ANATAKATIFUZA.

Katika mwanzo 1; 1-2 tunasoma hivi; hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi, nayo nchi ilikuwa ukiwa tena utupu na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji. Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.

Tunaona kuwa uwepo wa dunia unakuja kwa tendo la ujio wa Roho ya Mungu. Vile vitu vikapata sura tena ya Mungu. Hivyo Roho huyo huumba upya na sala tunayosali hapa huwa na maana na sikuku ya leo ina maana hiyo pia. Je sura yetu kiroho na kimwili ikoje? Dunia yetu ya leo ina sura gani? Maisha yetu kwa ujumla yana sura gani? Mungu daima anaendelea kuumba - ni ipi nafasi ya Mungu katika uumbaji wa ulimwengu leo hii?

Ukweli wa kibiblia na zaidi kutoka mwinjili Yohani - unasema kuwa ufunuo wa Mungu kwetu unawezekana kwa sababu ya ufunuo wa upendo. Ni Roho Mtakatifu anayetuongoza na kutuwezesha katika ufunuo huo na hii inakuwa wazi pia katika kumfahamu Kristo na Neno lake. Ni roho atujaliaye hekima na busara ya Kristo na namna ya kuona. Ni roho inayotuwezesha kuwepo ulimwenguni kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ni huu uwepo wa fumbo, huu muungano na Mungu unaomwezesha mwanadamu kuwepo.

Masomo yetu ya leo yanatupa mwanga juu ya habari ya Roho Mtakatifu. Lengo la Mtakatifu Luka kuandika injili na kitabu cha matendo ya mitume ni kuonesha kwa ujumla hali halisi ya Ukristo.

Pendo la Mungu linalookoa ni kwa kila mmoja, kila mahali na kwa kila kizazi. Chombo cha utendaji katika kuenenda huko ni Roho Mtakatifu. Mwinjili Luka anaweka wazi jambo hili - angalia injili ya leo habari juu ya nguvu ya Roho Mtakatifu.

Mtakatifu Luka anaelewa wazi kuwa huu ndio mwanzo wa kanisa na wajibu wake katika kutangaza habari njema kwa njia na nguvu ya Roho Mtakatifu.

Katikasomo la kwanza Mtakatifu Petro anaonesha wazi Roho huyu anatolewa kwa sababu ya kazi ya wokovu ya Yesu Kristo - Mdo. 2;32-33. Yesu huyo Mungu alimfufua na sisi sote tu mashahdi wake. Basi yeye akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu na kupokea kwa Baba ile ahadi ya Roho Mtakatifu amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kusikia. Roho Mtakatifu analeta pendo la wokovu wa Kristo kwetu sisi. Ndiye Roho huyu tunayepaswa kumpokea na kutenda naye kazi kama wakristo na katika maisha yetu ya kikristo kila siku. Kinyume chake ipo hatari ya kuishi roho zetu na si roho wa Mungu aliyetumwa kwetu toka pendo la Mungu Baba na mwanae Kristo.

Kwetu sisi tunaoamini - tunaweza kuamini na kushuhudia kwa sababu ya uwepo wa huyo roho. Roho huyo anafanya kazi ndani mwako/yangu/mwetu.

Katikasomo la pili - Mtakatifu Paulo anasema hakuna awezaye kumwita Bwana isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Ukristo wako/wetu ni mpango wa Roho katika kueneza ufalme. Pentekoste imetokea kwako.

ROHO MTAKATIFU ANA NAFASI GANI KATIKA MAISHA YAKO AU UNAMWELEWAJE ROHO MTAKATIFU? JE UNATAMBUA UWEPO WAKE? JE WEWE UNAYE ROHO MTAKATIFU AU UNAISHI MAISHA NA ROHO MTAKATIFU? ROHO MTAKATIFU NI MTENDAJI.

Katika barua ya Mtume Paulo kwa Wakorintho twaona tabia mbili za kazi ya Roho Mtakatifu.
    Ugawaji wa mapaji maalumu kwa waamini na zaidi tukiendelea Paulo anaorodhesha mapaji hayo. Mengine ni ya pekee kabisa kama kuongea kwa ndimi lakini mengine ni ya kawaida ya kutekeleza katika maisha yetu ya kikristo ya kila siku kama kufundisha, kusaidia wengine kwa hali na mali na kuongoza wengine. Muhimu hapa kila tufanyacho tukisaidiana katika kweli na haki huonesha nguvu ya Roho Mtakatifu ikifanya kazi ndani yetu ni zawadi yake. Na namna ya kutambua kuwa kama tumepokea zawadi hii au tunaishi zawadi hii ni kama tu inawasaidia wengine au kama asemavyo mtume Paulo kwa ajili ya faidi ya wote. Zawadi za Roho Mtakatifu ni kwa wale wote waaminio. Ndo maana mtume Paulo anasema kuwa zawadi kubwa kabisa ya huyo roho ni UPENDO.
  1. Tabia ya pili ya Roho Mtakatifu ni nguvu ya kuunganisha. Roho huyo huumba upya katika roho moja. Sote tumebatizwa katika mwili mmoja. Wakati kila mkristo amepewa karama yake na roho huyo wote tumekuwa mwili mmoja katika Kristo. Roho Mtakatifu anatuunganisha sote.

  2. a. Roho Mtakatifu huonekanaje? Gal. 5: 18-23 – mkiongozwa na Roho hamkai chini ya sheria. Matendo ya mwili yanatambulikana wazi; ndiyo haya; uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, ucheza mazingaombwe, uadui, ugomvi, kijicho, hasira, ubinafsi, utengano, mafarakano, wivu, ulevi, ulafi na mengineyo kama hayo. …. Lakini matokeo ya Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, hisani, ukarimu, upole, kiasi. Hakuna sheria inayopinga hayo.


b. Kwa namna ya pekee pia injili ya leo yaunganisha uwepo wa Roho Mtakatifu wa msamaha dhambi. Roho Mtakatifu anahusishwa moja kwa moja na msamaha wa dhambi. Mitume wanapewa uwezo wa kusamehe dhambi. Lakini pia kwa namna ya pekee kila wakati ambapo sisi tunasameheana kati yetu tunatenda hilo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Hii ni faida kubwa ya ujio wa Roho Mtakatifu na maana mojawapo ya kufurahi tunapoadhimisha sherehe ya PENTEKOSTE.

c. Ndugu mpendwa imani yako kwa Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu ni zawadi ya utumishi hata kama ni ndogo kiasi gani. Umoja wako na wengine, uwezo/utayari wako wa kusema nakusamehe kwa yule aliyekosea yote haya ni alama ya uwepo wa Roho anayetenda kazi ndani yako. Nenda kafanye hayo/sote tukatende hayo na Roho Mtakatifu ataonekana kati yetu. Huyo Roho si hewa au maneno mazuri yasiyokuwa na matendo makuu ya Mungu. Tuishi na kutenda fundisho linavyotuagiza.

Tunaomba.
    Hekima - uwezo wa kupambanua kwa njia ya akili mema na mabaya. Kupambanua ukweli na uongo ili kutoa hukumu kadiri ya sheria ya Mungu.

Hek. 9,1 sala ya kumwomba Mungu hekima – nakusihi unipe hekima ambayo huketi karibu nawe………….

Katika Lk 21;15 Yesu anapozungumzia dalili za dhuluma na za ushuhuda anasema kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga.
    Akili - kutoa kweli kwa muono wa kina na kupenya kwenye ukweli wa Mungu.
  1. Shauri – ili nishike njia nzuri

  2. Nguvu - kushinda magumu au kuvumilia mateso kwa nguvu na uwezo toka kwa Mungu.

  3. Elimu - kuamua kwa usahihi juu ya kweli za imani kadiri ya chimbuko halisi na kanuni za kweli zinazofunuliwa.

  4. Ibada - kumwona Mungu kuwa Baba wa wote.

  5. Uchaji wa Mungu – unaodai usikivu


Imeandaliwa na Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.