Ile hali ya kufanya kazi kwa mazoea iliyojengeka kwa baadhi ya watendaji wa Serikali
leo imewatokea puani watendaji wa Manispaa ya Dodoma wakati Waziri Mkuu wa Tanzania
Mizengo Pinda alipoamua kufanya ziara kukagua miradi ya maendeleo. Akiwa katika eneo
la kwanza ambalo alipangiwa kukagua ujenzi wa kituo cha afya cha Mkonze Jumamosi,
Juni 7, 2014 Waziri Mkuu alipokea taarifa ya ujenzi wa kituo na kubaini kuwa hawajafanya
chochote ili kutekeleza maagizo yake aliyoyatoa Machi 22, 2014.
Katika taarifa
yake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe alimweleza Waziri
Mkuu kwamba walifanya tathmini ya ujenzi wa kituo hicho na kubaini kuwa zinahitajika
sh. Milioni 24.15 na kwamba maombi ya matumizi hayo yamepangwa kujadiliwa kwenye kikao
cha kamati ya fedha na uongozi kitakachofanyika Juni 10, mwaka huu.
Akiwa katika
maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji ambayo Kitaifa yalifanyika mkoani Dodoma, Waziri
Mkuu alizindua mradi wa maji jirani na kituo cha afya cha Mkonze na kubaini kuwa kuna
hitilafu za ujenzi. Ndipo akaagiza kwamba ufanyike ukarabati na yeye akaahidi kuja
kukagua ukarabati huo mwezi Juni, 2014.
Mara baada ya kusomewa taarifa ya mradi,
Waziri Mkuu akahoji ni kwa nini hawajafanya chochote tangu alipotoa maelekezo Machi,
mwaka huu. Hakupata jibu la kueleweka kutoka kwa viongozi wa wilaya na mkoa. Waziri
Mkuu aliwasalimia wananchi waliokuwepo kwenye eneo hilo na kuwaeleza kwamba hawezi
kukagua kituo hicho ilhali hakuna kilichotekelezwa tangu afike hapo Machi mwaka huu.
Alisema
haiwezekani yeye atoe maagizo katika kipindi chote hicho halafu kisifanyike kitu chochote.
Akaondoka na kuendelea na ziara hadi kijiji cha Manzase ambako alikagua mradi wa kisima
cha maji.
Mapema, katika taarifa yake, Mhandisi Kilembe alisema kituo hicho
cha afya kilijengwa chini ya ufadhili wa ubalozi katika makubaliano yaliyofikiwa Novemba
11, 2009 kwamba ingetoa dola za marekani 84,307 sawa na sh. Milioni 152.86. Hata hivyo,
mara baada ya ujenzi kukamilika Agosti 29, 2012, kituo hicho kilipata nyufa nyingi
hali iliyosababisha kifungwe na wananchi walitoa malalamiko yao kwa Waziri Mkuu Machi
mwaka huu wakati alipokwenda kuzindua mradi wa maji kwenye kijiji cha Mkonze jirani
na kituo hicho.