2014-06-07 07:12:13

Ebo! Wewe ni nani?


Sikukuu ya Pentekoste inafunga kipindi cha Pasaka kilichodumu kwa muda wa siku hamsini. Katika kipindi chote tumeuishi mwanga wa ufufuko ulioupatia umaana na hatima ya maisha na uwepo wetu hapa duniani.

Kichwa cha Injili ya leo kinasema: “Wanafunzi wanamwona Bwana:” Neno hili linamaanisha kuona kitu kwa undani zaidi ya unavyoweza kuhakiki ambako macho ya kawaida hayawezi kuona. Kadhalika haisemwi kwamba “Yesu alijitokeza,” bali “Yesu alionekana”. Kwa hiyo hata wewe unaweza kumwona ukiwa na moyo safi, kama alivyosema Yesu mwenyewe: “Heri wenye moyo safi maana watamwona Mungu,” yaani hata sisi tunaweza kuiona hatima ya maisha tuliyopewa.

Aidha, Injili inasema: “Yesu akasimama katikati,” Yaani alionekana amesimama katikati yao. Haisimulii juu ya kutokea na kutoweka kwa Yesu, bali “yupo katikati.” Huo ni uwepo mpya na wa kudumu wa Yesu kwa jicho la imani, kwamba sasa anakaa katikati ya wanafunzi wake yupo nao na anatanguzana nao katika safari yao ya maisha.

Baada ya kuwepo hivyo katikati yao anawaambiwa: “Amani kwenu.” Na baada tu ya amkio hilo zuri, Yesu akatoa ID (Identity Card) yake, yaani vitambulisho vyake na kuwaonesha ili kuwathibitishia kuwa kweli ni yeye. Wote tungetegemea kuona Yesu anavichomoa toka mfukoni mwa kanzu yake vitambulisho vyenye picha ya sura yake kama ni halali na sura wanayoiona au ni feki, au vitambulisho amevigushi.

Kumbe, kinyume cha mategemeo yetu sote Yesu “akawaonesha mikono yake na ubavu wake.” Yesu anaonesha kitambulisho cha mikono iliyotobolewa misumari alipopigiliwa msalabani; na ubavu uliotobolewa kwa mkuki. Ni ukweli ulio bayana, kwamba hadi leo hii ukimwuliza mtoto mdogo au mtu wa dini yoyote ile akuambie Yesu alikuwa nani? Atakusimulia kuwa “Yesu ni mtu aliyewahi kuishi hapa duniani lakini aliuawa kwa kutundikwa msalabani mikono na miguu na baada ya kufa pale msalabani wakamtoboa ubavu kwa mkuki.” Hivi ndivyo vyeti vinavyomtambulisha Yesu kuwa ni nani, alifanya nini na kwa ajili ya nani alifanyiwa hivyo.

Hebu tujiulize zaidi hivyo vitambulisho vinamaanisha nini? Kadiri ya fikra za watu wa nchi za mashariki hata kadiri ya fikra zetu za kiafrika, mikono inamaanisha uwezo, mamlaka, nguvu–kazi ambazo mtu anafanya. Mikono inatumika kufanya kazi za kujenga na kubomoa. Mathalani, waswahili tumezoea kusikia mtu anayefaidi chakula baada ya kazi aliyofanya tunasema: “anakula kazi ya mikono yake.” Mgeni anayekufikia bila zawadi anaambiwa “amefika mikono mitupu.” Mwizi anaitwa “ana mkono mrefu”; au bahili tunamwita “ana mkono wa birika au mkono mfupi”; Zamani kidogo aliyekuwa anaomba rushwa alikuwa anasema: “hebu nipige ngumi kidogo”.

Wakati mwuaji au anayedhulumu wengine anaambiwa “mikono yake inanuka damu.” Sheria au utaratibu wa nchi unaitwa “mkono wa dola” nk. Kadhalika katika Maandiko Matakatifu ya Agano la Kale, mikono ilitafsiriwa pia kwa namna chanya au hasi: “Kuangukia mikononi mwa Mungu” kuliweza kumaanisha kuwa katika ulinzi wa Mungu, lakini pia iliweza kuwa, kulaaniwa na Mungu na hivi: “huwezi kuepuka mkono wa Mungu”. Yasemwa pia Mungu alikuwa anafanya kazi au kupigana vita kwa mikono yake na hivi tunasema uumbaji ni: “kazi ya mikono ya Mungu.”

Kwa hiyo katika mikono anayeonesha Yesu tunaweza kuutafakari maana yake katika imani na dini yetu, na hasahasa kuutafakari ufunuo wa nguvu ya mikono ya Mungu. Mosi, mikono ya Yesu imesubilibiwa kwa sababu amejitoa mwenyewe kabisa kwa ajili ya kumtumikia binadamu, ni kama anatuambia: “mikono hii haikuja ili kuwapiga na kulipiza kisasi wale wanaonipiga kwa mikono yao, bali mimi ninawapenda tu hata kama ninyi mtatumia mikono yenu kunipiga na kunisulibisha.” Huu ndiyo upendo wa Mungu. Pili, mikono ya Mungu inajitoa kufanya shughuli za kawaida za kibinadamu. Mathalani, tunaiona mikono Yesu inaiosha miguu michafu ya mitume.

Kule Nazareti tunaiona mikono ya Yesu ikitenda mambo mengi: Mikono ya Yesu iliwagusa na kuwaponya wakoma, ilifungua macho ya kipofu, mikono ilimponya yule mwanamke aliyekuwa amepinda, mikono ilimwinua aliyepooza, mikono ya Yesu iliwakumbatia watoto wadogo hadi mitume kukwazwa kwa vile watoto si wasafi, nk. Kijumla mikono ya Yesu iliwahudumia watu wote bila ubaguzi: wazee, vijana, akina mama, wanaume, watoto, vilema, vipofu, viziwi, bubu, wakoma, wenye pepo, nk. Hiyo ndiyo nguvu ya mikono ya Mungu, inafanya matendo ya Mungu ya kuwatendea mema watu wote.

Huu ndiyo ufunuo wa mikono ya Mungu kwa njia ya Kristu, anayetuonesha leo mikono yake ili mikono yetu pia ifafanane na mikono ya Mungu. Tukiwa kama watoto wake tulioumbwa kwa mikono yake, na kukombolewa kwa mikono yake, nasi pia tuwe na mikono kama hiyo yake. Watoto wa Mungu ni wale wanaofanya kazi ile ile iliyofanyika na Yesu, ambayo ni kazi na mikono ya Mungu mwenyewe.

Kitambulisho kingine anachokionesha Yesu ni ubavu uliotobolewa kwa mkuki hadi kuugusa moyo. Moyo ni alama ya kupenda au kuchukia kitu. Mathalani ukipenda unasema: “moyo wangu unapenda”, kama hutaki, unasema: “moyo wangu haupendi” au “moyo mweusi”. Maana yake, moyoni ndiko kunakokaa mawazo na fikra za kupenda au kutopenda, kama inavyosema Biblia juu ya kutupenda Mungu: “mawazo ya moyo wake ni kwa kizazi hata kizazi.”

Kwa hiyo, ubavu unaonesha upendo halisi wa Mungu. Ni upendo peke yake unaoweza kutuonesha uso halisi wa Mungu. Jeraha lile la kwenye moyo ni kilele cha upendo wa Mungu kwetu. Sisi tunapotaka kuonesha upendo, tunauchora moyo kama kitambulisho cha upendo. Kumbe, ID au kitambulisho cha upendo wa Yesu kinaonekana katika jeraha la ubavuni. Jeraha hilo ndilo linafanya historia ya mpenda. Majeraha haya mawili yatabaki daima kuwa kitambulisho cha kudumu cha upendo wa Mungu kwetu.

Baada ya kuupitia mchakato huu wa kuhakiki vitambulisho vya Yesu, tunaambiwa kwamba “wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.” yaani wamefunguka macho yao, wanaonekana kujitambua kuwa hivyo ndivyo sasa ni pia vitambulisho vyao vya kazi. Kwa hiyo kinachofuata ni kutumwa kufanya kazi. Ndiyo maana Yesu anawaagiza: “Kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi.” Kazi hiyo ya utume imeanza kwa Baba kisha akamrithisha Mwanae aliyeuonesha uso wa Baba yake kwa vitambulisho vya majeraha yake.

Sasa mitume wanatumwa ili kuendeleza na kuonesha katika ulimwengu kuwa wao ndiyo wanaobeba vitambulisho hivyo halali vya chama, nao ndiyo wanachama wake hai. Wako tayari kuonesha vitambulisho hivyo katika ulimwengu bila woga wala aibu na kuvitendea kazi.

Yesu akiwa binadamu kama sisi bila aibu na woga wowote amefanikiwa kuonesha vitambulisho vyake vya upendo. Kwa hiyo, kazi tunayotumwa sisi ni ile ya kujitoa zawadi sisi wenyewe, kwanza kumdhihirisha Yesu mfufuka kwa ulimwengu bila kumwonea aibu. Yesu ametupenda na kutuheshimu sana hadi kuthubutu kuturithisha sisi vitambulisho vyake.

Kwa unyenyekevu wote tupokee kazi hiyo ya Yesu, tukikumbuka kuwa ni kwa nguvu ya roho yake tu tunaweza kuvitumia vitambulisho hivyo na kuvitendea kazi. Ndivyo anavyoendelea kuwafanyia na kuwaambia mitume wake: “Pokeeni Roho Mtakatifu”. Kuvuvia huko ni kama kule ambako Mungu alimpulizia uhai mtu wa kwanza alipomwumba. Kadhalika leo Yesu anaumba upya.

Baada ya uumbaji huo mpya anawatuma kazi anapowaambia: “Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.” Kwa sentensi hii kumewekwa Sakramenti ya kitubio, lakini maana siyo hiyo tu, bali inamhusu kila mmoja kumwepusha mtu aliyepotoka na kumweka katika njia sawa.

Yesu ametupatia sisi sote uwezo wa kuondoa dhambi, kuacha dhambi, na tung’ae ule mwanga wa ufufuo aliotuachia. Hilo ni jukumu kubwa katika maisha yetu. Daima kuufanya Ufalme wa Mungu nukue dani mwetu na ndani ya wengine kwa kumshuhudia Yesu kwa njia ya Roho wake tuliyempokea. Tunafundishwa leo kutokugushi vitambulisho au kutokuwa na uso feki (uso wa kinafiki) unaofuata imani au dini feki. Kadhalika tusiwe na mkono mrefu kuuzidi urefu wa mkono wa dola au sanasana mkono wa Mungu. Jihadhali pia mikono yako isinuke damu ya kupokea rushwa na kudhulumu wengine. Kufanya hivyo ni kuwa na sura feki na ID au vitambulisho vya dini feki.

“Roho ya Kristo initakase,
mwili wa Kristu uniokoe,
damu ya Kristu initakase,
maji ya ubavu wa Kristu yanioshe,
Mateso ya Kristu yanitie nguvu,
Ee Yesu mwema unisikilize.
Unifiche ndani ya jeraha yako,
Usikubali nitengane nawe,
Uniite saa ya kufa kwangu,
Nikusifu pamoja na watakatifu wako,
Milele na milele. Amina.”

P. Alcuin Nyirenda








All the contents on this site are copyrighted ©.