2014-06-06 15:03:18

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amtembelea Papa mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 6 Juni 2014 amekutana na kuzungumza na Bwana Lech Walesa na ujumbe wake kutoka Poland. Viongozi hawa wameshirikishana masuala mbali mbali ya kimataifa na kitaifa. Baba Mtakatifu pia amekutana na kuzungumza na Waziri mkuu wa Japan Bwana Shinzo Abe pamoja na ujumbe wake mjini Vatican ambao wamejadili masuala ya msingi katika medani za kimataifa. Waziri mkuu wa Japan amelishukuru Kanisa kwa msaada wake wa hali na mali wakati Japan ilipokumbwa na Tsunami

Waziri mkuu wa Japan amemzawadia Baba Mtakatifu Francisko kioo cha muujiza kilichokuwa kinatumiwa na Wakristo wakati wa madhulumu ili kuonesha Msalaba na Sura ya Yesu kinapokutana na Mwanga. Amemzawadi pia Picha ya Balozi wa kwanza wa Japan aliyefika mjini Vatican kunako mwaka 1615 ili kuomba msaada wa Wamissionari kutoka katika Kanisa Katoliki, ili kusaidia mchakato wa Uinjilishaji nchini Japan na Picha ya Pili inamwonesha Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI, ambaye Waziri mkuu aliwahi kukutana naye katika maisha yake!

Baba Mtakatifu Pia amepatia mgeni wake zawadi ya medali ya Mtakatifu Petro alipokuwa anaokolewa kutoka Gerezani kama inavyooneshwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume 12: 1-17.

Waziri mkuu wa Japan Bwana Shinzo Abe amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na ujumbe wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.