Seminari ni mahali ambapo majandokasisi wanafundwa kiroho, kiakili, kiutu, kimaadili
na kitamaduni kwa kutambua kwamba, wanahimizwa kuwa karibu zaidi na Kristo katika
maisha na utume wao kwa njia ya Sala, Sakramenti na tafakari ya kina ya Neno la Mungu.
Katika majiundo
yao ya awali na endelevu majandokasisi watambue kwamba, wanaitwa kumfuasa Kristo kwa
karibu zaidi na kwamba, wako huru kuitikia wito huo na kuanza kuambatana na Yesu,
au kuukataa na kuendelea na mipango mingine ya maisha.
Kwa jandokasisi anayekubali
mwito wa kumfuasa Kristo kama Padre anapaswa kutambua anachangamotishwa kuonesha ile
taswira ya Yesu mchungaji mwema anayejisadaka kwa ajili ya huduma, ustawi na maendeleo
ya Kanisa la Kristo. Hii ndiyo changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Kardinali Fernando
Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wakati wa ziara yake
ya kikazi nchini Cameroon kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 100 ya Ukristo
Jimbo kuu la Bamenda, kwenye Seminari kuu ya Nkolbisson, Jimbo kuu la Yaoundè, Cameroon.
Seminari hii ina majando kasisi 120 wanaojiandaa kwa ajili ya wito na maisha ya kipadre.
Kardinali
Filoni amewataka waseminari katika majiundo yao ya Kikasisi kuwa kweli ni mashahidi
wa Injili ya Furaha kama anavyohimiza Baba Mtakatifu Francisko; vyombo muhimu katika
utekelezaji wa kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Yesu Kristo mwenyewe. Wao wanapaswa
kuwa ni Kristo mwingine, “Alter Christus”, mabalozi waaminifu na wa kweli kati ya
watu, wanaoshiriki katika mchakato wa mabadiliko ya maisha yanayopaswa kuanzia kwa
majandokasisi wenyewe!
Majandokasisi wajifananishe na Kristo katika kila ngazi
ya maisha yao: kibinadamu, kiakili, kiroho na katika masuala ya kichungaji. Mambo
haya yanatekelezeka kwa njia ya sala ya kijumuiya na sala binafsi, Yesu daima akiwa
ni dira na mwelekeo wa maisha. Majiundo haya yanaboreshwa na kurutubishwa kwa njia
ya Sakramenti za Kanisa hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti
ya Upatanisho inaymwonjesha mwamini upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani.
Tunu hizi muhimu katika majiundo ya kikasisi, zitawawezesha kweli kuwa ni wachungaji
wanaopeta katika upendo na huduma kwa Familia ya Mungu.
Ili kweli majandokasisi
waweze kuwa ni mashahidi wa wa Injili ya Furaha hawana budi kuachana kabisa na tabia
ya unafiki, kwa kuonesha ukomavu katika hisia, kwa kutokumbatia wala kukumbatiwa na
malimwengu na hatimaye, kuonesha moyo wa umoja na mshikamano katika huduma. Upadre
ni daraja la huduma kwa ajili ya Fanmilia ya Mungu na matunda ya kazi hii yanategemea
kwa kiasi kikubwa mshikamano walio nao na Kristo mwenyewe ambaye ni kichwa cha Fumbo
la Mwili wake, yaani Kanisa. Ni matunda yanayotegemea jinsi ambavyo waliweza kumwilisha
tunu mbali mbali katika mchakato wa majiundo yao ya Kipadre.
Majandokasisi
wanapaswa kutambua changamoto zinazowakabili Mapadre katika maisha na utume wao, ili
kuwa tayari kukabiliana nazo katika azma ya Uinjilishaji Mpya. Waseminari waige mifano
bora ya maisha na utume wa Kipadre, waendelee kujielekeza katika utakatifu wa maisha
kwa kumpenda Kristo na jirani zao kama njia ya kulijenga na kuliimarisha Kanisa!
Imehaririwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.