Kumsadiki Roho Mtakatifu ni kukiri Nafsi ya tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, atokaye
kwa Baba na Mwana na anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana. Huyu ndiye
Roho Mtakatifu aliyetumwa mioyoni mwa waamini, ili kupokea uzima mpya wa wana wateule
wa Mungu.
Katika Fumbo
la Utatu Mtakatifu usiogawanyika, Mwana na Roho ni Nafsi tofauti lakini hawatenganiki.
Tangu mwanzo hadi mwisho wa nyakati, Baba anapomtuma Mwanaye, anamtuma pia Roho wake
anayewaunganisha na Kristo kwa imani ili waamini wakiwa wamefanywa waana waweze kumwita
Mungu, Abba, yaani Baba.
Siku hamsini baada ya ufufuko wake nidyo Siku kuu
ya Pentekoste, Yesu Kristo aliyetukuzwa mbinguni alimmimina Roho Mtakatifu pasi na
kipimo, akamdhihirisha kuwa Nafsi ya Kimungu, hivi kwamba, Fumbo la Utatu Mtakatifu
limefunuliwa kikamilifu. Utume wa Kristo na ule wa Roho Mtakatifu vilikuwa utume wa
Kanisa, lililopelekwa litangaze na kueneza Fumbo la Umoja wa Utatu Mtakatifu.
Kwa
ufupi, Roho Mtakatifu anajenga, anahuisha na kutakasa Kanisa. Roho Mtakatifu anawarudishia
Wabatizwa hali ya kufanana na Mungu iliyopotezwa kwa njia ya dhambi na anawafanya
waishi ndani ya Kristo uzima uleule wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Anawatuma washuhudie
ukweli wa Kristo na kuwapanga katika kazi zao maalum, ili wote wazae tunda la Roho.
Hili
ndilo Fumbo ambalo linatarajiwa kuadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Siku
kuu ya Pentekoste, Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican kuanzia saa 4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya, kadiri ya taarifa iliyotolewa na
Monsinyo Guido Marini Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa.