Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linawataka waamini na watu wote wenye mapenzi
mema kuunganisha nguvu zao, ili kujenga umoja na mshikamano, tayari kusaidia familia
zinazoteseka kutokana na myumbo wa uchumi wa kitaifa. Mshikamano huu, unapaswa kujionesha
katika maisha ya kiroho na kimwili. Ni changamoto inayotolewa na Askofu Michael Dixon
Bhasera, Rais wa Baraza la Maaskofu katoliki Zimbabwe.
Akizungumza na Baraza
la Maaskofu Katoliki Zimbabwe hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko aliwapongeza
Maaskofu kutoka Zimbabwe kwa kuwa karibu na wananchi wao wakati wa shida na raha;
kabla na baada ya kupata uhuru na hasa zaidi pale maelfu ya wananchi wa Zimbabwe walipolazimika
kuikimbia nchi yao kwa kukata tamaa na kukosa mwelekeo kutokana na machafuko ya kisiasa
nchini Zimbabwe yaliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Watu wengi
walipoteza maisha na kwa hakika watu walimwaga machozi.
Zimbabwe ni nchi ambayo
ilikuwa imefikia kiwango kikubwa cha maendeleo lakini machafuko ya kisiasa, yamevuruga
maendeleo ya kiuchumi kiasi kwamba, wananchi wengi bado wanaogelea katika dimbwi la
umaskini; mmong'onyoko wa kimaadili na hali ya kukata tamaa. Yote haya ni mambo yanayojikita
katika miundo inayojikita katika dhambi binafsi na dhambi jamii. Kumbe, kuna haja
ya wananchi wa Zimbabwe kufanya toba na wongofu wa ndani kwa kuchuchumilia utakatifu
wa maisha.