2014-06-06 15:28:32

Kumekucha!


Baba Mtakatifu Francisko, Rais Shimon Peres wa Israel pamoja na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina, Jumapili jioni wakiunga na viongozi mbali mbali wa kidini wanatarajiwa kusali kwa pamoja katika Bustani za Vatican ili kuombea amani huko Mashariki ya Kati.

Tukio hili la Sala linatarajiwa kufanyika majira ya jioni. Tukio hili linatarajiwa kuhudhuriwa pia na Patriaki Bartolomeo wa kwanza aliyepewa mwaliko na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Nchi Takatifu. Ni muda wa sala, tafakari na nyimbo za kidini.

Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa vatican anabainisha kwamba, mara tu baada ya sala na tafakari Marais wataondoka kuelekea mahali walipofikia, lakini Patriaki Bartolomeo wa kwanza ataendelea kubaki na Baba Mtakatifu kwenye makazi yake ya Santa Martha, mjini Vatican.

Padre Pierbattista Pizzaballa mhudumu mkuu wa Maeneo Matakatifu katika Nchi Takatifu anasema, hii si sala ya kiekumene wala mchakato wa kutafuta suluhu ya kisiasa kati ya Palestina na Israeli, bali ni muda wa kusali na kutafakari kwa pamoja kuhusu umuhimu wa amani huko Mashariki ya Kati. Ni Sala ya Kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uumbaji. Sehemu ya pili ni kutambua udhaifu wa binadamu na hivyo kumwomba Mungu msamaha na sehemu ya tatu ni kuombea amani katika Nchi Takatifu.








All the contents on this site are copyrighted ©.