2014-06-06 09:18:22

Dumisheni amani!


Jumuiya ya Kimataifa inaposherehekea kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kusitishwa kwa Vita kuu ya Pili ya Dunia, viongozi wa Kanisa nchini Ufaransa wanaadhimisha tukio hili kwa njia ya sala, kwa kuwakumbuka askari wote waliojisadaka kwa ajili ya kutetea haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa anasema kwamba, anaungana na wote wanaoendelea kuombea amani bila kuwasahau askari wote waliopoteza maisha kutokana na Vita kuu ya Pili ya Dunia.

Ni wajibu wa vijana wa kizazi kipya kutambua na kuheshimu sadaka iliyotolewa na mashujaa waliosimama kidete kupinga utawala wa kinazi, changamoto na mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wakiwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vya watu, ili kweli Injili ya Kristo iweze kushika mkondo wake ili kukuza na kudumisha amani, udugu na mshikamano. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia hija njema ya amani wakiendelea kuombewa na Mtakatifu Bernadetha wa Msalaba, Msimamizi mwenza wa Bara la Ulaya.All the contents on this site are copyrighted ©.