2014-06-06 14:57:43

Changamoto kwa Askari ni ukweli na huduma!


Askofu Santo Marcianò wa Jimbo la Kijeshi nchini Italia katika Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Carabinieri nchini Italia, amewashukuru wanajeshi hawa wanaotekeleza kazi yao kwa kuzingatia weledi, uhakika, majitoleo na sadaka ya kweli kutoka moyoni!

Ni kipindi cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, ili kurudi katika asili ya Jeshi hili, tayari kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoibuliwa katika uilimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hizi ni changamoto zinazofumbatwa katika ukweli na huduma; mambo yanayojikita katika maamuzi ya maisha, kwa kusimama kidete na kutetea ukweli, hata kama utawagharimu mateso, kifungo au kifo. Askari lazima wajiepushe na vitendo vya rushwa ili kusimamia ukweli.

Ili kudumisha ukweli wa kisayansi kuna haja pia kwa Askari kufanya uchunguzi wa kina ili kubainisha ukweli wa matukio mbali mbali yanayoendelea katika jamii kutokana na ukosefu wa uhuru, vita na mauaji ya kimbari, kiasi kwamba, kuna baadhi ya familia zinapoteza maisha wakati zikiwa gerezani! Ukweli unafumbatwa katika undani wa maisha ya mwanadamu; ni ukweli huu unaopaswa kutolewa ushuhuda kwa njia ya zawadi ya maisha, kwa kulinda na kuheshimu zawadi ya maisha, utu na heshima ya binadamu

Askari ni huduma kwa ajili ya raia na mali zao pamoja na mafao ya wengi. Kuhudumia maana yake ni kupenda na kupenda maana yake ni kutoa huduma makini kadiri ya wito na hali ya Carabinieri. Askari hawa waendelee kuwa waaminifu kwa utume na nchi yao! Upendo kwa Mungu na jirani uwe ni dira ya utekelezaji wa majukumu yao kama Askari!







All the contents on this site are copyrighted ©.