2014-06-05 15:52:33

Wakristo wanahitaji imani na matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 5 Juni 2014 amekutana na kusali pamoja na Patriaki Aram wa kwanza, Katolikos wa Armenia pamoja na ujumbe wake pamoja na kuwatakia amani wanapotembelea makaburi ya wataktifu Petro na Paulo kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa, ili kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya Wakristo.

Baba Mtakatifu anampongeza Patriaki Aram wa kwanza kutokana na juhudi zake katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ya Baraza la Makanisa pamoja na Makanisa yaliyoko Mashariki ya Kati yanayokabiliana na changamoto na magumu ya maisha. Ameendelea kutoa mchango wa hali na mali kwa Wakristo walioko katika maeneo haya pamoja na kuchangia katika Tume ya majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox yaliyoko Mashariki.

Baba Mtakatifu anaonesha matumaini ya kufikia umoja kamili miongoni mwa Wakristo kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi ya Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake, ili wote wawe wamoja! Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kukabiliana na mateso wanayoyakubali kwa ujasiri kwa ajili ya upendo kwa Mungu. Wakristo wa Kanisa la Kitume la Armeni wamejikuta wakiwa ni mahujaji wanaotembea kuelekea katika Ufalme wa Mungu.

Waarmeni ni watu ambao wamekumbana na historia ya uhamiaji, dhuluma na mauaji ya kidini, kiasi cha waamini kubaki wakiwa na madonda makubwa mioyoni mwao, kielelezo cha Madonda Matakatifu ya Yesu, imani na matumaini kwa huruma na upendo wa Mungu. Kanisa linahitaji imani na matumaini kwa ajili ya Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati, hasa miongoni mwa wale wanaoishi katika maeneo yenye vita, vurugu na kinzani za kijamii. Wakristo wanahitaji fadhila hizi ili wasimsahau Mwenyezi Mungu na kujikuta wanatumbukia katika kinzani kati yao wenyewe au kusahau vita dhidi ya dhambi.

Wakristo wajifunze kusaidiana kwa unyenyekevu, huku wakitembea katika upendo kama Kristo alivyowapenda wao na kujisadaka kwa Mungu kama sadaka safi isiyokuwa na mawaa! Wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, hapo ukawa ni mwanzo wa Kanisa, Waamini wanahamasishwa kumwomba Roho Mtakatifu chanzo cha maisha, ili aweze kuiumba upya dunia, kuponya majeraha na kuleta upatanisho miongoni mwa watu pamoja na Muumba wao.

Mwishoni Baba Mtakatifu anamwomba Roho Mtakatifu awaongoze katika hija ya umoja kamili ndani ya Kanisa kwa kuwafundisha namna ya kujenga na kuimarisha udugu unaopata chimbuko lake katika Ubatizo na imani moja.







All the contents on this site are copyrighted ©.