Umoja na utume wa Kanisa ni nyenzo muhimu katika maisha ya Kanisa
Patriaki Aram wa kwanza wa Kanisa la Kitume la Armenia amemshukuru Baba Mtakatifu
Francisko kwa moyo wa upendo, urafiki na udugu na kwamba, hii ni mara yake ya tatu
kutembelea Vatican na kuonana na Mapapa tangu mwaka 1997, kielelezo cha mshikamano
katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa haya mawili.
Kuanguka
kwa utawala wa Armenia kunako mwaka 1375 kumepelekea makundi makubwa ya wananchi wa
Armenia kuikimbia nchi yao na kujikuta wameenea sehemu mbali mbali za dunia, changamoto
ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa ili kukabiliana na changamoto
za kichungaji, ili hatimaye, umoja kati ya Wakristo uweze kuonekana wazi na Kanisa
kutoa ushuhuda wa pamoja. Kanisa la Kitume la Armenia litaendeleza majadiliano ya
kitaalimungu na Makanisa mengine duniani, kwani umoja na utume wa Kanisa ni mambo
yanayoshibana.
Patriaki Aram wa kwanza amempongeza Baba Mtakatifu Francisko
kwa kujisadaka katika kuwatangazia Maskini Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuendelea
kutetea utu na heshima ya binadamu, kielelezo cha ushuhuda wa kimissionari, changamoto
kubwa kwa Kanisa kwa nyakati zote. Haki na amani ni changamoto nyingine inayopewa
kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko na hili pia amempongeza kwa juhudi
hizi.