2014-06-05 07:54:33

Mwaka wa Watawa Duniani 2014 - 2016


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufungua na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Mwaka huu utafunguliwa rasmi hapo tarehe 30 Novemba 2014 Domenika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio na kufungwa rasmi tarehe 2 Februari 2016, siku ya Watawa Duniani. RealAudioMP3

Haya yamebainishwa katika mkutano wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa uliofanyika hivi karibuni mjini Roma kwa kuongoza na kauli mbiu “kuuamsha ulimwengu. Watawa katika utume wa Kanisa la leo.” Wakuu wa Mashirika wametakiwa kuendelea kuzifanyia kazi changamoto na ushauri uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na wakuu wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume.

Wakuu wa Mashirika wanaendelea kuchangamotishwa kufanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Mashirika yao kwenye Makanisa mahalia, kwa kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, hasa wanapotembelea nyumba za mashirika yao kadiri ya sheria na kanuni za Kanisa. Wamekubaliana kwamba, watachangia tafakari ya kina kuhusu maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, mjini Vatican pamoja na kutoa mwelekeo wa maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani: 2014 – 2016.

Maandalizi haya yanafanyika katika awamu kuu tatu: sehemu ya kwanza ni maadhimisho yatakayofanywa katika ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Maadhimisho haya yatakwenda sanjari na mikakati itakayopangwa na wakuu wa Mashirika na baadaye maadhimisho yatayofanyika kwenye Makanisa mahalia kwa kuyahusisha Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika maeneo yao.

Ratiba elekezi iliyotolewa na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume inaonesha kwamba, tarehe 29 Novemba 2014 kutafanyika kesha la sala kwa ajili ya kuzindua Mwaka wa Watawa Duniani. Tarehe 30 Novemba 2014, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufungua Mwaka wa Watawa Duniani kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Wakati wa Juma la kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 24 Januari 2015 kutafanyika kongamano la kiekumene kimataifa kwa kuwaalika watawa kutoka Mashirika mbali mbali ya kitawa nje ya Kanisa Katoliki. Tarehe 8 hadi tarehe 11 Aprili 2015 kutafanyika kongamano la kimataifa kwa ajili ya walezi katika maisha ya kuwekwa wakfu, lengo ni kubainisha vigezo vinavyoibuliwa katika tasaufi ya maisha ya pamoja.

Tarehe 23 hadi tarehe 26 Septemba 2015 kutafanyika kongamano la watawa vijana. Juma la maisha ya kitawa litaadhimishwa kuanzia tarehe 24 Januari hadi tarehe 2 Februari 2016 na hapo Baba Mtakatifu atafunga rasmi Mwaka wa Watawa Duniani. Kwa ujumla hii ndiyo ratiba elekezi itakayotumika kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani 2014 hadi mwaka 2016.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.