Baba Mtakatifu Francisko anawaomba waamini wa Makanisa ya Kiorthodox na Kikatoliki
Barani Ulaya, kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini, kwa kuheshimiana
na kuthaminiana kama ndugu wamoja katika Kristo, ili kuwamegea wengine matumaini katika
maisha.
Huu ni ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliowandakia wajumbe
wanaoshiriki katika Jukwaa la nne la majadiliano ya kiekumene kati ya Waorthodox na
Wakatoliki, majadiliano yaliyofunguliwa hapo tarehe 2 na yanafungwa rasmitarehe 6
Juni 2014, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Dini natofauti za kitamaduni: changamoto kwa
Makanisa Barani Ulaya". Jukwaa hili limeandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
Katoliki Barani Ulaya kwa kushirikiana na Makanisa ya Kiorthodox yaliyoko Barani Ulaya.
Ujumbe huu umeandikwa na Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican kwa
niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anayewapongeza wahusika wakuu kwa kuendeleza jitihada
za majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa, ili kuimarisha umoja na mshikamano,
ili kulinda na kutetea uhuru wa kidini, kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Mkutano
huu unaendelea kujadili masuala ya kibinadamu, mikakati ya kichungaji, masuala ya
kijamii na kimaadili.
Mkutano huu unafanyika kwa faragha kwa kuangalia kwa
namna ya pekee masuala ya kidini na tamaduni Barani Ulaya; tunu msingi za maisha ya
Kikristo na umuhimu wake katika jamii ya nyakati hizi; uhuru wa kidini, mchango wa
Makanisa katika kukuza na kuendeleza hekima ya Kikristo pamoja na majadiliano ya kidini
yanayopania ujenzi wa misingi ya maadili na utu wema miongoni mwa wananchi wa Bara
la Ulaya. Jukwaa hili linahudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Kanisa la Kiorthodox
na Kanisa Katoliki.
Wajumbe wanaendelea kukazia umuhimu wa kujenga na kudumisha
misingi ya haki, amani na utulivu; wamewaombea wananchi wa Ukraine wanaokabiliana
na machafuko ya kisiasa kwa wakati huu. Kuna haja ya kuheshimiana hata katika tofauti
zinazojitokeza katika masuala ya kidini na kitamaduni, kwani Bara la Ulaya lina utajiri
mkubwa wa watu kutoka katika kabila, lugha na jamaa; wote hawa wanahistoria, lugha
na tamaduni zao. Changamoto za Kikristo hazipanii kung'oa tamaduni za watu, bali kuwasaidia
watu kujitamadunisha zaidi kwa kuzingatia kweli za Kiinjili.