Kardinali Mauro Piacenza, mhudumu mkuu wa Toba katika barua yake kwa mapadre waungamishaji
anasema kwamba, kila mara Mkristo anapoungama dhambi zake na kupokea msamaha, huruma
na upendo wa Mungu kutoka kwenye kiti cha maungamo, kwa Mkristo hii ni Pentekoste
Mpya! Siku kuu ya Pentekoste, hii ni fursa kwa waamini kujipatanisha na Mungu pamoja
na jirani zao, ili kuweza kumpokea vyema Roho Mtakatifu anayemiminwa mioyoni mwao,
tayari kumtolea Mwenyezi Mungu ushuhuda wa maisha adili na matakatifu!
Neema
ya Sakramenti ya Upatanisho anasema Kardinali Piacenza ni mang'amuzi mapya ya Pentekoste
kwani hapa Roho Mtakatifu anaendelea kulitakasa Kanisa la Kristo kwa njia ya huduma
ya maungamo inayotolewa na Padre akiwa ameungana na Yesu Kristo, ili kusikiliza na
kupima, kuamua na kutoa ushauri na hatimaye, kuponya dhambi kwa kumwondolea mwamini
dhambi zake. Hii ni kazi ya Roho Mtakatifu anayetenda kwa njia ya wachungaji wake
wanaojisadaka katika viti vya maungamano.
Mapadre wanakumbushwa kwamba, wamechaguliwa
na kuwekwa wakfu kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu si kwa mastahili yao wenyewe
bali kwa njia ya neema ya Roho Mtakatifu inayowaunganisha kwa dhati kabisa na Kristo
mwenyewe, ili kushiriki upendo na kazi yake ya ukombozi. Kwa sababu hii, Padre ni
mhudumu wa huruma ya Mungu na daraja kati ya waungamaji na Kristo mwenyewe.
Mapadre
wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa wasikivu kwa Roho Mtakatifu na karama zake
zinazoliwezesha Kanisa kujitakasa na kuwatakatifuza watoto wake kwa njia ya Sakramenti
ya Upatanisho!