Kanisa liwe ni sura ya furaha na ukarimu kwa Zingari
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 5 Juni 2014 amekutana na kuzungumza na wajumbe
wanaoshiriki katika kongamano la kimataifa linalojadili kuhusu mikakati ya shughuli
za kichungaji kwa Zingari, kongamano linaloongozwa na kauli mbiu "Kanisa na Zingari:
Kutangaza Injili pembezoni mwa jamii. Hii ni kumbu kumbu kati ya Jumuiya ya Waamini
na Zingari na historia inayolenga watu kukutana na kufahamiana ili kwa pamoja waweze
kujielekeza zaidi katika mapambano dhidi ya changamoto zinazojitokeza kati shughuli
za kichungaji lakini zaidi katika Uinjilishaji Mpya.
Zingari ni watu ambao
wanaishi pembezoni mwa Jamii na mara nyingi ni kundi ambalo halipendwi na wengi na
wanawaangalia kwa mashaka makubwa. Kimsingi hakuna sera makini za kisiasa, kiuchumi
na kijamii zinazojielekeza kwa ajili ya kuasaidia watu hawa. Zingari nao wanahamasishwa
kushiriki katika kuchangia katika mafao ya wengi, kwa kuwajibika, kutekeleza nyajibu
zao na kuendeleza haki msingi za wote.
Ukosefu wa miundo mbinu makini ya elimu
na majiundo ya kitamaduni ni kati ya mambo ambayo yanaweza kuwatumbukiza baadhi ya
watu ndani ya jamii katika lindi kubwa la umaskini, magonjwa, ubaguzi katika soko
la ajira pamoja na kutothaminiwa. Ikiwa kama mambo haya ni kati ya madonda makubwa
ya kijamii, basi wanyonge watajikuta wakitumbukizwa kwa urahisi katika mifumo mbali
mbali ya utumwa mamboleo, kwani hawa ni watu ambao hawana ulinzi na usalama wa kutosha.
Zingari ni kati ya makundi ya watu wanaoendelea kutumbukizwa katika utumwa
mamboleo, kwani hawashirikishwi na wala utu wao hauheshimiwa kiasi kwamba, wanashindwa
kuishi kama raia wengine.
Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linatumwa kuwatangazia
watu Injili ya Furaha na hii ndiyo changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi na Mama
Kanisa kwa ajili ya maskini na wote wanaosukimzwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa lioneshe
mshikamano wa upendo kwa kufuata ushuhuda ulioneshwa na Yesu Kristo, Mwana mpendwa
wa Baba.
Mshikamano huu uungwe mkono na taasisi za kitaifa na kimataifa, kwa
kubainisha miradi na mbinu za kuboresha maisha. Utu na heshima yao vipewe msukumo
wa pekee pamoja na kuibua mbinu na mikakati mipya kutoka katika medani mbali mbali
za maisha sanjari na kuweka mipango ya kichungaji inayotekelezwa na Mama Kanisa kutokana
na changamoto zinazojitokeza katika mtindo wa madhulumu, ukandamizaji na hata wakati
mwingine utumwa!
Baba Mtakatifu anawahimiza wajumbe na wadau mbali mbali kujielekeza
zaidi katika kuwasaidia na kuwahudumia wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ya
mwanadamu. Zingari wapate ndugu wanaowapenda kama Kristo alivyowapenda wale waliokuwa
wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa liwe kweli ni sura ya furaha na ukarimu
kwa Zingari.