2014-06-05 11:35:04

Kanisa halina haja na wapangaji!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu aliyoadhimisha kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, Alhamisi tarehe 5 Juni 2014 anasema kwamba, Kanisa liko huru na kamwe halifungwi na watu wenye misimamo mikali ya kiimani au Wakristo wanaotafuta mafao yao binafsi au wakristo wasiokuwa na mwelekeo; watu ambao ni sawa na bendera fuata upepo! Kwa waamini kama hawa, hawana nafasi ya kudumu ndani ya Kanisa ni sawa na wapangaji tu, watu wa mpito!

Baba Mtakatifu anasema, Yesu kabla ya kuondoka kwenda mbinguni kwa Baba yake, aliwaombea wafuasi wake ili waweze kudumu katika umoja, kumbe, wale wanaotaka kuligawa na kulichafua Kanisa hawana nafasi, changamoto kwa kila mwamini kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linaundwa na watu wenye karama, maoni na vipaji mbali mbali kwa ajili ya mafao ya ustawi wa Kanisa, mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Roho Mtakatifu aweze kutenda kazi yake na kuwajengea waamini uwezo wa kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia. Watu wenye misimamo mikali ya kiimani ni hatari hata ndani ya Kanisa ni watu wasiopenda mabadiliko!

Kanisa daima limeonesha unyenyekevu na uvumilivu mkubwa kwa Watoto wake, lakini kuna baadhi ya waamini anasema Baba Mtakatifu ni wale wanaotafuta njia mbadala; watu wasiojisikia kuwa kweli ni sehemu ya Kanisa; ni watu wenye mawazo pengine hata kinyume cha Mafundisho tanzu ya Kanisa, lakini wao pia wanajiita Wakristo! Hatari kubwa!

Baba Mtakatifu anasema kuna watu wanaingia Kanisani kwa ajili ya kutafuta mafao yao binafsi, hali ambayo ilijionesha tangu mwanzo wa Kanisa, lakini wote hawa walikiona cha mtema kuni! Hata leo hii wapo waamini wa aina hii Maparokiani, Majimboni na hata ndani ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Ni watu wanaotafuta mafao na faida binafsi. Watu kama hawa ni wapangaji!

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa haliwahitaji wapangaji, linawataka Wakristo wanaojisikia kuwa kweli ni sehemu muhimu sana ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa na wanashiriki katika ujenzi wake kwa njia ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha. Kanisa linatambua karama na mapaji ya Roho Mtakatifu miongoni mwa watoto wake. Kuna haja ya kutambua tofauti msingi katika maisha na karama ndani ya Kanisa kwani hii ni kazi ya Mungu mwenyewe. Waamini wajenge utamaduni wa kujinyenyekeza ili kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu, ili aweze kuwakirimia amani na utulivu!







All the contents on this site are copyrighted ©.