Mahali popote pale utakapokuwa wakati wa kusherehekea Siku kuu ya Pentekoste, itakapo
gota saa 7: 00 mchana, inamisha kichwa chako, sali kidogo kwa ajili ya kuombea amani
Mashariki ya Kati, kadiri ya imani na Mapokeo yako ya kidini ukiwa umeungana na Baba
Mtakatifu Francisko. Ni changamoto inayotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina.
Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kwa namna ya pekee, kusali
kwa ajili ya kuombea jitihada za Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya upatikanaji
wa amani huko Mashariki ya Kati. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko atakutana
na kusali pamoja na Marais kutoka Palestina na Israeli kama sehemu ya utekelezaji
wa mwaliko kwa viongozi hawa wawili wakati wa hija yake ya kitume katika Nchi Takatifu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawaalika waamini na watu wote wenye
mapenzi mema, wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kusali kwa ajili ya kuombea
amani huko Mashariki ya Kati.