2014-06-04 12:19:49

Papa kutembelea Hospitali ya Gemelli 29 Juni 2014


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa katika maadhimisho ya Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu hapo tarehe 27 Juni 2014 kutembelea Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, kilichoko mjini Roma sanjari na maadhimisho ya siku 90 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki.

Kardinali Pietro Parolin katika barua aliyomwandikia Kardinali Angelo Scola, Rais wa Taasisi ya Gemeli Toniolo anasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahimiza wadau mbali mbali kushirikiana kwa dhati katika kuimarisha Chuo Kikuu cha Kikatoliki, kwa ajili ya mafao ya wengi. Anatambua mchango unaotolewa na Kitivo cha tiba na upasuaji kilichoko Hospitali ya Gemelli wakati huu kinaposherehekea Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Kitivo hiki kimeendelea kuwa ni msaada mkubwa kwa ajili ya tiba kwa wagonjwa kwa kuthamini na kuheshimu utu wa binadamu. Kutokana na mchango huu, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko wa kutembelea Hospitali ya Gemelli ili kuzungumza na wafanyakazi pamoja na kusalimiana na wagonjwa wanaolazwa Hospitalini hapo.

Kardinali Angelo Scola katika ujumbe wake kama sehemu ya maandalizi ya tukio hili amewaandikia wanafunzi wa kitivo cha tiba na upasuaji cha Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, kutokubali kamwe kupokonywa matumaini yao na wala wasithubutu kutafuta njia za mkato katika maisha, bali waoneshe ujasiri wa kupambana na magumu pamoja na changamoto za maisha kwa kujikita katika majiundo makini ya kitaaluma na tafiti mbali mbali.

Tangu kuanzishwa kwake, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu kimekuwa ni mtekelezaji mkuu wa utume wa Kanisa katika kuwafunda vijana taaluma sanjari na kuendeleza mchakato wa majadiliano kati ya imani na uwelewa wa mwanadamu, ili kuwapatia vijana wa kizazi kipya ufahamu makini kwa kujichotea hekima na busara kutoka kwa Yesu Kristo, chemchemi na busara yote ya kimungu katika maisha ya mwanadamu!All the contents on this site are copyrighted ©.