2014-06-04 14:47:10

Paji na uchaji wa Mungu ni kielelezo cha upendo na imani!


Mama Kanisa anafundisha kwamba, Mapaji Saba ya Roho Mtakatifu ni: Hekima, Akili, Shauri, Nguvu, Elimu, Ibada na Uchaji wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi zake, ameendelea kufanya tafakari ya kina kuhusu Mapaji Saba ya Roho Mtakatifu na, Jumatano tarehe 4 Juni 2014 ametafakari Paji la Uchaji wa Mungu, zawadi ya maisha ya kiroho, inayomkirimia mwamini upya wa maisha, furaha, shukrani na upendo ambao Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu kwa njia ya Yesu Kristo!

Baba Mtakatifu anasema ni katika mahusiano haya kunajengeka msingi mkamilifu na ibada ya kweli kwa Mwenyezi Mungu. Upendo ambao umemiminwa mioyoni mwa waamini kwa njia ya Roho Mtakatifu unawawezesha kuona uwepo na upendo wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao na hivyo kujibu kwa furaha katika sala na kuabudu.

Uchaji wa Mungu si mambo yanayojionesha kwa nje, bali ni moyo wa kweli wa ibada unaomfanya mwamini kumrudia Mungu kama Baba yake na kuendelea kukua na kukomaa katika upendo kwa jirani kwa kuwaona na kuwatambua wengine kuwa ndugu na jamaa moja ya Familia ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba Paji la Uchaji wa Mungu kutoka kwa Roho Mtakatifu, ili waweze kuwa tayari daima kuwasaidia wengine katika furaha na utambuzi wa mshikamano unaopata chimbuko lake katika umoja na Mwenyezi Mungu pamoja na Fumbo la Mwili wake yaani Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Siku kuu ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia mitume na kuwapatia mapaji yake, waamini wamwombe Roho Mtakatifu Mapaji yake, ili kweli waweze kuwa ni mashahidi wa upendo wa Mungu unaojikita katika furaha. Anawatakia amani na baraka tele katika maisha yao ya kila siku. Katika shida na changamoto za maisha, waamini wamwombe Roho Mtakatifu ili awajalie Paji la Uchaji wa Mungu ili kuendelea kuwa ni mashahidi wa imani ya Kikristo, umoja na mshikamano na Mungu pamoja na jirani.

Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa namna ya pekee vijana kutoka Poland ambao wamekusanyika huko Lednica nchini Poland, ili kurudia ahadi zao kwa Kristo na Kanisa lake kwenye Kisima cha Ubatizo, wakitamani kuwa kweli ni watoto waaminifu, kwani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Wanataka kutafakari maana ya kuwa ni Watoto wa Mungu, ili kuonja upendo wake na kuutolea ushuhuda kati ya watu, wakionesha uaminifu kwa Mwenyezi Mungu ambaye amewapenda kwanza, akawaumba na kuwakomboa kwa njia ya Yesu Kristo.

Wanamshukuru Mungu kwa huruma na upendo wake wa kibaba, anayewafungua macho kuona mahitaji ya wengine na mwishoni, wanashiriki katika upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kushirikishana furaha, majonzi, mateso, maendeleo hata pale wanapokosa mafanikio.

Hii ni hija ya maisha ya kiroho iliyozinduliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II miaka kumi na minane iliyopita mjini Lednica; awaongoze na kuwasaidia kupata neema ambazo wanahitaji ili kufikia ukamilifu wa maisha yao ya ujana pamoja na kuonesha ukarimu. Amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kudumisha amani na udugu.







All the contents on this site are copyrighted ©.