Masista wa Maria Imakulata wanapenda kuwakaribisha ninyi nyote wanapotafakari mwaka
wa Mtumishi wa Mungu Padre Yohane Schneider ambao ulifunguliwa rasmi tarehe 07-12-2013
na utafungwa tarehe 07-12-2014 ukiongozwa na kauli mbiu “kuiishi karama ya mwanzilishi
katika mazingira tunamoishi na kufanya kazi”.
Huu ni mwaliko
ambao unatupatia nafasi ya kutafakari zaidi na kwa kina maisha ya Mtumishi wa Mungu,
baba mwanzilishi wetu Padre Yohane Schneider. Hakika Maisha ya mwanzilishi wetu ni
chachu ya maisha yetu.
Shirika la Maria Imakulata lilianzishwa mnamo mwaka
1854 huko Wroclaw, nchini Poland, na Mtumishi wa Mungu Padre Yohane Schneider. Shirika
lilisajiliwa na kupata hati ya Kipapa tarehe 22 Desemba 1897 lilithibitishwa na hatimaye
kupewa Hati ya Sifa. Hivyo tunapokumbuka miaka 160 tangu kuanzishwa kwa Shirika letu
tumeona ni vema kama familia moja ya Wana Immakulata kukaa chini na kutafakari fadhili
ambazo Mungu anatukirimia siku kwa siku bila ya mastahili yetu. Kwetu imekuwa ni tendo
la shukrani kwa Mungu kwa wema na upendo wake kwetu sisi Watawa wa Shirika la Immakulata.
“Saidieni
kuokoa roho za mabinti zilizo karibu na genge la uharibifu...” ni wosia wa mwanzilishi
wetu ambao ndio maneno ya msingi katika Karama ya Shirika letu, yaani kuwasaidia wasichana
na akina mama walio na maisha duni ili waweze kumtambua Mungu na kuuishi utu na Ukristo
wao kwa kutimiza wajibu na majukumu yao ndani ya jamii katika misingi ya haki na
upendo.
Kwa njia hiyo, mbegu ya Shirika letu ilipandwa na hatua kwa hatua Shirika
linaendelea kukua na kusambaa katika mabara na nchi mbalimbali duniani. Masista wa
Maria Immakulata wanafanya kazi katika Bara la Ulaya, Asia na Afrika; katika bara
la Afrika tupo Tanzania na tunafanaya kazi katika Jimbo katoliki la Tunduru- Masasi
katika Parokia ya Chikukwe ambamo ipo nyumba ya malezi ya Wanovisi.
Pia tunafanya
kazi katika Parokia ya Nanjota na ipo nyumba ya malezi ya wakandidati na wapostulanti.
Katika Jimbo kuu la Dar es Salaam tunafanya kazi katika Parokia ya Kurasini na ndipo
ilipo nyumba Mama ya Shirika katika kanda ya Tanzania. Baadhi ya Masista wanafanya
kazi katika ubalozi wa Vatican nchini Tanzania.
Vilevile tunafanya kazi katika
Jimbo la Same katika Parokia ya Mwanga na pale ni Kituo cha kiroho na kielimu kwa
Masista wetu. Pia tunafanya kazi katika Parokia ya Kilomeni. Kwa jinsi hiyo, tunaweza
kusema siri kuu ya mafanikio yetu ni Sala na Kazi ambamo tunakutana na Kristo mpole,
mnyenyekevu na mwenye huruma, tunapotoa huduma kwa wazee, akina mama, vijana, maskini,
wagonjwa na watoto, pia tupofundisha dini shuleni na utume wetu Parokiani. Hivyo basi,
tunapoendelea kumshukuru Mungu naweza kusema kwamba: Zawadi ya sala yetu ni Amani,
Upendo na Furaha, kwani mikono yetu tunaitumia kwa kazi, na mioyo yetu tunaiinua
kwa Mungu.
Miito ya kitawa: Shirika la Masista wa Maria Imakulata linapokea
wasichana wote wenye wito na utayari wa kuokoa Roho zilizopo katika genge la uaribifu
ambao wana elimu yoyote yaani baada ya darasa la saba.
Je unapenda kujiunga
nasi?
Tuandikie Murugenzi wa Miito Shirika la Masista wa Maria Imakulata S.
L. P 47, Same. Kilimanjaro-Tanzania.