Mfumo dume unavyokwamisha mapambano dhidi ya Ukimwi
Imeelezwa kuwa mikakati ya Serikali ya Tanzania katika kupambana na kuondoa mfumo
dume bado unakumbwa na vikwazo kutokana na mfumo huo kuhamia katika mapambano dhidi
ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi. Taarifa hiyo imesema wanaume walio wengi
mkoani Mbeya wanawatumia wake zao kama 'sample' ya majibu ya kufahamu afya zao baada
ya kuwatuma kwenda kupima peke yao katika vituo vya upimaji wa hiari, zahanati, vituo
vya afya na hospitalini.
Hayo yamesemwa na Mnasihi wa ushauri nasaha kuhusu
mapambano ya virusi vya ukimwi na ukimwi, Shirika la misaada ya Kanisa Katoliki Caritas
Mbeya, kituo cha Iyunga, jijini Mbeya, Alex Kumwenda wakati akitoa taarifa katika
kikao cha mpango kazi cha kila mwisho wa mwezi. Bwana Alex ametoa ushauri kwa wafanyakazi
kuwa wa kwanza kuonesha mfano kwa jamii ili nao waweze kuiga na kwamba tatizo hilo
limeingia hadi katika masuala ya uzazi ambapo wanaume licha ya kushauriwa kuwasindikiza
wenzi wao bado wanakwepa.
Msimamizi wa waelimishaji rika caritas Teddy Haizenje
amesema upo umuhimu wa kuwatumia waelimishaji rika katika Kata mbalimbali ili kuelezea
umuhimu wa kusindikizana kwa wenza katika kupima afya zao kwa pamoja na madhara ya
kupima na kuamini usalama kwa majibu mwanaume au mwanamke.
Naye Ofisa ugani
wa Caritas Parokia ya Igurusi, wilayani Mbarali, Luckson Mwakilindile ameshauri kufanyika
kwa kampeni maalum ya kuielimisha jamii faida ya kushiriki kwa pamoja kupata majibu
ya afya zao ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza baada ya kupokea majibu kwa
upande mmoja ikiwemo kuandaa matamasha,semina na makongamano kwa kushirikiana na wafadhiri
mbalimbali.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Idara ya caritas na maendeleo Jimbo katoliki
la Mbeya, Edgar Mangasila amesema kutoa ripoti haitoshi na kwamba kama shirika wanapaswa
kushirikiana na jamii wanayofanya nayo kazi katika kuielimisha na kuihamasisha umuhimu
wa mume na mke kwenda kwa pamoja kupima kwa hiari.
"Ili ni jukumu letu sote
na tulione hili ni tatizo,hivyo tunapaswwa kwa umoja wetu kila mmoja katika mahali
pake pa kazi ashirikiane na jamii husika kutoa elimu na kuhamasisha umuhimu wa kwenda
pamoja kupima kwa hiari afya....hii ya kutoa tu ripoti haitoshi lazima tubebe utajiri
wa kuhakikisha tunapata ufumbuzi wa kutatua tatizo hili katika jamii yetu,"amesema
mangasila.
Ameongeza Mkurugenzi huyo,"mabwana shamba lazima muwashirikishe
wakulima huko mnakofanya nao kazi, wasimamizi wa masuala ya wanawake,jinsia na watoto
nanyi kw anafasi yenu huko mlipo,wahasibu,waratibu sote tunawiwa na jamii hii kuiokoa
na kuondoa magumu na makando kando yanayojitokeza."
Kikao cha mpango kazi katika
Idara ya Caritas Jimbo Katoliki la Mbeya kinafanyika kila mwisho wa mwezi ambapo wafanyakazi
wanaanza kwa kukutana kwa idara husika katika kikao cha awali kufanya mang'amuzi ya
utume wao ambapo siku inayofuata wanakutana katika vitengo vyote kutoa taarifa za
kazi zilizofanyika kwa mwezi husika na mpango kazi wa mwezi unaofuata.
Katika
kikao hicho pia alitambulishwa mfanyakazi wa kujitolea kutoka nchini Italia, Chiara
Cantoni anayefanya kazi na Mbeya Community Based rehabilitation program for Children
with Disabilities (Mbeya CBR- Simama) wanaoshirikiana na Caritas Jimbo la Mbeya.
Chiara
naye alitoa ripoti kutoka CBR-Simama ambapo alishukuru kwa moyo wa upendo na ushirikiano
alioukuta kwa wafanyakazi wa Caritas na ameahidi kushirikiana kwa pamoja kwa hatua
zote.