2014-06-04 06:53:53

Jubilee ya miaka 25 ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Poland


Uhuru na mshikamano ni mambo msingi wakati huu Poland na Vatican zinapofanya kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 25 tangu nchi hizi mbili zilizpoanzisha uhusiano wa Kidiplomasia, mambo muhimu pia wakati huu wa mabadiliko makubwa katika medani za kisiasa na kijamii.

Mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Poland katika historia ya miaka ya hivi karibuni ni kielelezo makini cha utashi wa wananchi wa Poland kutaka mabadiliko ya dhati yanayojikita katika uhuru na mashikamano wa kweli, hali iliyopelekea kuanguka kwa ukuta wa Berlin, hapo ukawa ni mwanzo mpya wa maisha ya wananchi wa Poland.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka 25 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Poland na Vatican, huko Varsavia. Uhuru wa kidini ni mwendelezo wa mambo msingi katika maisha ya wananchi wa Poland yanayojionesha katika katiba na Sheria za Kimataifa.

Uhuru wa kidini ni jambo ambalo limeendelea kupewa kipaumbele cha pekee katika mabadiliko yanayojitokeza nchini Poland, ili kuwawezesha watu kujenga misingi ya imani na matumaini thabiti sanjari na utekelezaji wa demokrasia ya kweli dhidi ya vitendo vya kutovumiliana, ubaguzi na misimamo mikali ya kidini, mambo ambayo yanapaswa kukemewa na kuoneshwa kwamba, hayafai kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu.

Kanisa linaheshimu na kuthamini kazi zinazotekelezwa na Serikali na kwamba, ushiriki wake katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Poland unajikita katika uhuru wa kuabudu pamoja na utekelezaji wa haki msingi za binadamu, ili kudumisha amani na utulivu. Utekelezaji wa uhuru wa kuabudu kwa namna ya pekee unahitaji kuongozwa na kanuni auni na mshikamano.

Katika ziara yake ya kichungaji nchini Poland, Kardinali Pietro Paroli tarehe 1 Juni 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kielele cha Jubilee ya miaka 25 ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Poland na Vatican; ibada ambayo imehudhuriwa pia na viongozi wa Kanisa na Serikali kutoka Poland. Amewakumbusha waamini kwamba, ushindi wa uhuru wa kidini umepatikana kwa njia ya Msalaba. Kumbe, hakuna sababu ya kuwa na wasi wasi, licha ya ukosefu wa fursa za ajira, tatizo la watu kukimbia nchi yao na watu kutokuwa na uhakika wa maisha yao kwa siku za usoni, mambo ambayo yanayumbisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Kardinali Pietro Parolin anawataka wananchi wa Poland kujiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kwa maombezi yake, Mwenyezi Mungu aendeleee kutekeleza mpango wake kwa ajili ya familia ya binadamu. Mtakatifu Yohane Paulo II anaweza kuitwa kuwa ni msimamizi wa uhuru wa wananchi wa Poland.
All the contents on this site are copyrighted ©.