Upadre ni wito wa huduma unaotoa nafasi kwa Padre kumkumbatia Yesu moyoni mwake, tayari
kumpeleka kwa wengine katika ari na moyo mkuu, bila ya kujibakiza katika huduma kwa
maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Upadre si ujiko wala kazi!
Ni
maneno ya Baba Mtakatifu Francisko aliyowaandikia majandokasisi wanaojiandaa kuwa
Mapadre kutoka Cuba waliomwomba ushauri katika safari ya majiundo yao katika maisha
na wito wa kipadre. Baba Mtakatifu amewashukuru majandokasisi hawa kwa barua yao na
anawataka kusonga mbele kwa moyo mkuu pasi na kukata tamaa katika maisha na wito wao
wa Kipadre, ili hatimaye, siku moja waweze kuwa kweli ni Mapadre, wema na watakatifu
wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa Familia ya Mungu nchini Cuba.
Baba Mtakatifu
anawataka majandokasisi hawa wanaosoma katika Seminari ya Mtakatifu Basil Mkuu Santiago
di Cuba kujizatiti kweli kweli kwani inalipa kudumu hadi mwisho katika maisha na wito
wa Kipadre. Baba Mtakatifu anawataka Majandokasisi hawa kuonesha unyenyekevu na kupokea
kwa ukarimu: ushauri, mafunzo na majiundo yanayotolewa kwao na walezi wao.
Waseminari
wakubali kufundwa kiakili, kiroho, kimaadili, kiutu na katika mikakati ya shughuli
za kichungaji, wakikazia maisha ya kijumuiya ili kujenga na kuimarisha udugu na mshikamano
wa kipadre!