Rais Arthur Peter Mutharika wa Malawi baada ya kuapishwa anataka kuanza kuandika ukurasa
mpya wa Malawi kuhusiana na sera ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa
sanjari na kupambana na rushwa pamoja na ufisadi uliokithiri nchini Malawi.
Huu
ndio mwelekeo unaooneshwa na Rais Mutharika baada ya kuapishwa kuwa Rais Mpya wa Malawi
baada ya kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Malawi hapo tarehe
20 Mei 2014. Ni matumaini ya Rais Mutharika kwamba, viongozi wa vyama vya kisiasa
nchini Malawi watazika tofauti zao na kushikamana kwa ajili ya ujenzi wa Malawi mpya
inayosimikwa katika haki, demokrasia na maendeleo ya kweli!
Sherehe za kuapishwa
kwa Rais Mutharika zilihudhuriwa na wajumbe wengi kutoka ndani na nje ya Malawi, lakini
ni Rais Seretse Khana Ian Khama wa Botswana ndiye alihudhuria kama mkuu wa Nchi, jambo
ambalo limewashangaza wengi. Malawi inataka kuanzisha urafiki na nchi zinazoibukia
katika uchumi kimataifa kama vile Brazil, China, India na Afrika ya Kusini.