Hija za kitume zinazofanywa na Maaskofu Katoliki mjini Vatican walau kila baada ya
miaka mitano, zinalenga kuimarisha moyo wa sala, umoja na mshikamano na Khalifa wa
Mtakatifu Petro pamoja na kuendelea kujipyaisha katika maisha ya kiroho. Zimbabwe
ni kati ya Nchi ambazo ziko Kusini mwa Bara la Afrika, iliyofanikiwa kukuza na kuimarisha
ari na moyo wa kimissionari, kiasi cha watu kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya Kanisa nchini Zimbabwe.
Leo hii, Kanisa linaendelea kuvuna matunda ya sadaka
hii kutoka nchini Zimbabwe. Matunda haya yanajionesha kwa namna ya pekee katika huduma
zinazotolewa na Kanisa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu! Zimbabwe
imebahatika kuwa na idadi kubwa ya miito mitakatifu na kwamba, miito hii inaendelea
kukua na kuchanua, kielelezo cha neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, licha
ya changamoto zinazojitokeza, mwaliko wa kuendelea kudumu katika sala ya shukrani.
Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu
tarehe 2 Juni 2014 wakati alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki
Zimbabwe linalofanya hija yake ya kitume mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawapongeza
Maaskofu kwa kusimama kidete kulinda na kuwatetea wanyonge, wahamiaji na watu wasiokuwa
na makazi maalum. Watu wanaendelea kuteseka: kiroho, kimwili na kimaadili kutokana
na kushamiri kwa uwepo wa miundo ya dhambi, mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi
Mungu kwa kujikita katika maadili.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika kwa
namna ya pekee Maaskofu Katoliki nchini Zimbabwe kujibidisha katika ujenzi wa umoja
na uponyaji wa kitaifa katika medani mbali mbali za maisha zinazoundwa na makundi
ya watu nchini humo, ili kweli umoja uweze kujidhihirisha tena kwa kuendeleza mchakato
wa upatanisho wa kitaifa unaojikita katika upendo kwani uponyaji ni neema kutoka kwa
Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, wananchi wengi wa Zimbabwe wana madonda
makubwa, kiasi cha kuwakatisha tamaa. Kumbe, ni dhamana ya Maaskofu kuhakikisha kwamba,
wanawajengea wananchi wa Zimbabwe matumaini mapya kwani Kristo ameshinda dhambi na
mauti na mwanga daima utatawala katika maisha ya watu. Kanisa litaendelea kutangaza
Injili ya Matumaini nchini Zimbabwe, kwa wale waliopondeka na kuvunjika moyo, ili
waweze kuonja tena msamaha na huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa hasa
Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha ya Kikristo.
Baba
Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kuonesha unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu kwa
kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano na Mapadre wao sanjari na kutafuta na kukuza
miito mitakatifu. Maaskofu waendelee kuwasindikiza Mapadre vijana katika maisha na
wito wao wa Kipadre; kwa kuwasaidia katika kuhibiri na kuishi kadiri ya kweli za Kiinjili,
imani na mapendo kwa Mungu. Mapadre wajifunze kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya jirani zao, kwa kuonesha matumaini ya kinabii katika haki nchini Zimbabwe.
Baba Mtakatifu anasema, ustawi na maendeleo ya Kanisa nchini Zimbabwe na Afrika
katika ujumla wake kwa namna ya pekee kabisa unategemea majiundo makini kwa waamini
walei; Mapadre watakatifu pamoja na Makatekista waliofundwa kikamilifu wanaotolea
ushuhuda amini wa maisha yao ya Kikristo katika jamii inayowazunguka. Watawa wasaidiwe
kuitakatifuza Zimbabwe kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani zao. Wanandoa watarajiwa
waandaliwe kikamilifu kwa kuwashirikisha utajiri unaobubujika kutoka katika Mafundisho
adili ya Kanisa pamoja na upendo, ili waweze kuishi katika furaha na uhuru wa kweli
kama Baba na Mama.
Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni, amewataka Maaskofu Katoliki
kutoka Zimbabwe kuwaimarisha ndugu zao katika imani na umoja na kwamba, Khalifa wa
Mtakatifu Petro yuko pamoja nao katika kulihudumia Neno la Mungu, ili kweli Wakristo
nchini Zimbabwe waweze kuwa ni chumvi na mwanga wa mataifa Barani Afrika na duniani
kote.