Wamissionari waliotekwa nyara wako katika hali nzuri!
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu
wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Cameroon amekutana na kuzungumza na Wamissionari
watatu waliokuwa wametekwa nyara kwa takribani mwezi mmoja na hatimaye kuachiliwa
huru, Jumapili tarehe 1 Juni 2014. Kardinali Filoni anamshukuru Mungu kwa zawadi hii
kubwa kwa ajili ya Kanisa la Cameroon, ambalo lilikosa huduma za kiroho na kiutu zilizokuwa
zinatolewa na Wamissionari hawa nchini Cameroon.
Wamissionari waliokuwa wametekwa
nyara ni kutoka katika Shirika la Zawadi ya Roho Mtakatifu, Fidei Donum: Padre Gianantonio
Allegri na Padre Giampaolo Marta wote wawili kutoka Italia pamoja na Sr. Gilberte
Bussier kutoka Canada. Mapadre hawa wako katika hali nzuri: kisaikolojia na kiafya
na kwamba, wamesaidiana wakati wote walipokuwa wametekwa, lakini zaidi, wameonja uwepo
wa Kanisa zima kwa njia ya mshikamano wa sala na sadaka, kiasi kwamba, wakaendelea
kuwa na imani thabiti licha ya hofu na mashaka kuhusu hatima ya maisha yaliyokuwa
mikononi mwa watekaji nyara.
Serikali ya Cameroon bado inaendelea kufanya
uchunguzi wa kina ili kubainisha wale waliohusika na utekaji nyara huo, ili waweze
kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.