Ubia na sekta binafsi katika usafirishaji wa abiria!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za kwanza
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuingia kwenye ubia na sekta binafsi katika mradi
mkubwa wa usafirishaji abiria. Ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Juni 3, 2014 wakati
akifungua Mkutano wa Majadiliano yenye lengo la kuutangaza mradi wa mabasi yaendayo
kasi kwenye ukumbi wa Mlimani City. Mkutano huo wa siku mbili, utamalizika Jumatano,
Juni 4, 2014.
Waziri Mkuu amesema kutèkelezwa kwa mradi huo kutatoa fursa za
ubunifu utakaowezesha kupatikana kwa suluhisho la usafiri mijini na hasa kwenye miji
inakua kwa kasi barani Afrika. "Mbali ya kutoa huduma za hali ya juu, za haraka na
ambazo siyo ghali kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, nia ya Serikali ni kuona mfumo
mpya wa matumizi ya kadi kwenye mpango huu wa usafiri unatumika ipasavyo," alisema.
Alisema
ni matumaini ya Serikali kwamba wadau kutoka sekta binafsi ambao ni wazawa na wa kutoka
nje ya nchi watashiriki kwenye mradi huu ili uweze kuboresha matumizi ya kadi ambayo
mtu hatatakiwa kulipia fedha taslimu akiwa ndani ya basi bali kutumia kadi anayoilipia
kabla ya kuingia ndani ya basi husika.
Akizungumza na waandishi wa habari mara
baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Serikali iliamua kuanzisha mradi
huo ili kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara za Jiji la Dar es Salaam. "Hii
ni awamu ya kwanza ambayo inakaribia kukamilika na inaanzia Kimara hadi Kivukoni na
itakuwa na matawi mawili ya Morocco na Karikoo. Mradi wote una awamu sita za ujenzi
kuelekea maeneo tofauti ya Jiji," alisema.
Mbali na mradi huo wa mabasi yaendayo
kasi, Serikali inaangalia uwezekano wa kutumia usafiri wa majini kwa kutumia boti
kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari
jijini Dar es Salaam. “Vilevile tutaimarisha usafiri wa reli kama njia nyingie ya
kupunguza tatizo hili. Dk. Mwakyembe (Waziri wa Uchukuzi) ameanza na sote tumeona
ni jambo linalowezekana. Cha msingi ni kuimarisha tu usafiri huu,” aliongeza Waziri
Mkuu.
Mapema, akiwakaribisha wajumbe wa mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha
kuwa mradi huo unafanikiwa. Pia alitumia fursa hiyo kuishukuru Benki ya Dunia ambayo
alisema imetoa kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya kufadhili mradi
huo.
Mkutano huo unawashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wa ndani na wa
nje wanaotarajiwa kutoa huduma za mabasi makubwa na madogo, utoaji tiketi, ulinzi,
usafi na huduma za maduka.