2014-06-03 08:03:44

Mwanamke ni jembe la maendeleo!


Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, tarehe 16 Oktoba 2014 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, litatoa tuzo mbili zenye thamani ya Euro 10, 000 kwa kila kundi la wanawake ambalo limejifunga kibwebwe kuhakikisha kwamba, baa la njaa linapewa kisogo katika maisha yao.

Tuzo hii inakwenda sanjari na kampeni inayoongozwa na kauli mbiu “Wanawake ni vyombo vya maendeleo”, iliyozinduliwa hapo tarehe 8 Machi 2014 katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Wanawake sehemu mbali mbali za dunia wamekuwa daima mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya baa la njaa kwa kujikita katika uzalishaji wa mazao ya chakula kwa ajili ya familia zao na mazao ya biashara ili kujipatia uwezo wa kiuchumi.

Wachunguzi wa masuala ya wanawake na maendeleo wanasema kwamba, kuna wakati wanawake wanawajibika kufanya maamuzi machungu katika maisha yao kwa kuamua ni mtoto yupi apewe chakula wakati wa baa la njaa kama inavyojionesha nchini Syria na Sudan ya Kusini.

Wanawake waliojengewa uwezo katika uzalishaji wa mazao ya chakula na kilimo wamekuwa ni mfano wa kuigwa katika matumizi ya teknolojia rafiki kwa ajili ya kulinda na kutunza mazingira. Caritas Internationalis inaendesha kampeni dhidi ya baa la njaa duniani inayoungwa mkono na Baba Mtakatifu Francisko, ili watu waguswe na mahangaiko ya jirani zao!
All the contents on this site are copyrighted ©.