Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso kuanzia tarehe 26 hadi tarehe 29 Novemba
2014, litakuwa ni Mwenyeji wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi
katika mkutano unaolenga kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mapambano dhidi ya baa la
njaa duniani.
Huu ni mkutano
wa kimataifa unaolijumuisha Shirika la la Misaada la Kanisa Katoliki (OCADES) ambalo
ni tawi tanzu la Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa,
Caritas Internationalis. Mkutano huu utaongozwa na kauli mbiu “Mkakati wa kuondokana
na baa la njaa Ukanda wa Sahel”.
Mkutano huu utawashirikisha wajumbe kutoka
nchi za Afrika Magharibi na nje ya eneo hili kwa mwaliko maalum. Wadau mbali mbali
wanaojihusisha na haki msingi ya chakula katika ngazi ya kimataifa wamealikwa pia.
Hii itakuwa ni nafasi nzuri kwa Kanisa Afrika Magharibi kufanya upembuzi yakinifu
kuhusu baa la njaa na mikakati ya Kanisa katika mapambano haya sanjari na kufanya
mabadiliko msingi katika maisha ya jamii, ili baa la njaa usiwe tena ni wimbo usiokuwa
na kiitikio! Watu wawajibike katika kujihakikishia usalama wa chakula.
Itakumbukwa
kwamba, tukio hili ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya kimataifa inayotaka kuhakikisha
kwamba, watu wanakuwa na uhakika wa usalama wa chakula, iliyozinduliwa na Caritas
Internationalis kunako Desemba 2013 na Baba Mtakatifu Francisko akatoa ujumbe kwa
njia ya video, akiwahimiza waamini na watu wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu
katika kampeni hii kwani, baa la njaa bado ni kashfa kubwa duniani.
Inakadiriwa
kwamba, kuna watu billioni moja wanaokabiliwa na baa la njaa sehemu mbali mbali za
dunia, ingawa kuna uzalishaji mkubwa wa chakula! Ubinafsi, uchoyo na utandawazi wa
watu kutoguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zao ni chanzo kikubwa cha kuenea
kwa baa la njaa duniani!