Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 1 Juni 2014 ameshiriki katika kongamano
la kimataifa la Chama cha Uamsho wa Kikatoliki kwenye Uwanja wa Michezo wa Olympic
ulioko mjini Roma. Amesikiliza shuhuda za watu mbali mbali na kuombwa kutoa ushauri.
Kwa Mapadre amewataka kuwa karibu zaidi na Yesu Kristo kwa njia ya Sala, Tafakari
ya Neno la Mungu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Wawe karibu na Familia ya
Mungu wanayoihudumia kwa njia ya upendo kamili.
Baba Mtakatifu anawataka vijana
kutoka kifua mbele kutangaza Injili ya Furaha na kamwe ujana wao wasiufungie kwenye
makabati, kwani utachakaa kama soli ya kiatu na kukosa uzuri na matumaini. Ujana unapendeza
kwa kushirikishana na wengine ile furaha ya kukutana na Yesu Kristo pamoja na kujitoa
bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake!
Baba Mtakatifu amewakumbusha
wanafamilia kwamba, wao ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo palitoa fursa kwa
Yesu kukua, akaongezeka nguvu, akajaa hekima na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. Wanandoa
wapende kukuza na kudumisha upendo kati yao kwa kutambua kwamba, Shetani yupo na hapendi
kuziona familia zikistawi na kushamiri. Pamoja na udhaifu wao wa kibinadamu, wanandoa
waendelee kuwa thabiti katika imani kwa kuwarithisha watoto wao imani kutoka kwa Kristo
na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anaziombea Familia katika shida na magumu, changamoto
na fursa mbali mbali ziweze kudumu na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu zaidi.
Baba
Mtakatifu anasema wagonjwa na walemavu ni sehemu muhimu sana ya Kanisa, kwani wao
kwa namna ya pekee, wanaonja Fumbo la Mateso ya Kristo, changamoto ya kushuhudia imani
na matumaini hata katika mahangaiko yao ya ndani. Wazee nao wana nafasi kubwa katika
kurithisha imani kwa vijana wa kizazi kipya. Wazee waheshimiwe na kuthaminiwa katika
maisha na utume wa Kanisa, kwani ni kisima cha hekima na furaha ya kweli.
Mwishoni,
Baba Mtakatifu, amewaombea waamini waliokuwa wamekusanayika kwenye Uwanja wa Michezo
wa Olympic, huku wakiendelea kumsubiri Roho Mtakatifu, ili wajazwe nguvu ya Roho Mtakatifu
na kuwapatia zawadi ya kunena kwa lugha ya upendo na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Roho Mtakatifu awawezeshe kujenga na kudumisha umoja, upendo
na mshikamano wa dhati badala ya kuwa na uchu wa madaraka; awasaidie kuwa wanyenyekevu
na kulipenda Kanisa pamoja na kuwa na moyo wazi ili kupokea mapaji ya Roho Mtakatifu.