Kardinali Simon Duraisamy Lourdusamy, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili
ya Makanisa ya Mashariki aliyefariki duniani tarehe 2 Juni 2014 anatarajiwa kuzikwa
Alhamisi tarehe 5 Juni 2014 katika Ibada ya mazishi itakayoongozwa na Kardinali Angelo
Sodano, Dekano wa Makardinali na baadaye, Baba Mtakatifu Francisko atahitimisha kwa
Ibada ya Maziko.
Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za rambi rambi Askofu
mkuu Anthony Anandarayar wa Jimbo kuu la Pondicherry na Cuddalore kufuatia kifo cha
Kardinali Lourdusamy na kuwahakikishia wote walioguswa na msiba huu uwepo wake wa
karibu kwa njia ya sala na sadaka yake.
Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi
Mungu kwa maisha na utume wa Kardinali Lourdusamy, aliyejitosa kimasomaso kwa ajili
ya kutangaza Injili kwanza kabisa nchini India na baadaye kwa Kanisa la Kiulimwengu
akitekeleza dhamana mbali mbali hadi pale alipoteuliwa kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza
la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka 1999. Anamwombea
huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumkirimia amani na furaha ya mbinguni.
Baba Mtakatifu anatoa baraka zake za kitume kwa wote wanaoomboleza msiba huu mkubwa.
Marehemu Kardinali Lourdusamy alizaliwa kunako tarehe 5 Februari 1924 huko
Kalleri, India. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa tarehe
21 Novembe 1951. Tarehe 2 Julai 1962 akateuliwa kuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki
la Bangalore na kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 22 Agosti 1962. Tarehe 9 Novemba
1964 akateuliwa kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo kuu la Bangalore na kusimikwa hapo
tarehe 11 Januari 1968.
Tarehe 2 Machi 1970 atateuliwa kuwa ni Katibu mwambata
wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Tarehe 26 Februari 1973 akateuliwa kuwa
Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimissionari
ya Kipapa sanjari na kuwa ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana.
Mtakatifu
Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali tarehe 25 Mei 1985. Akateuliwa kuwa Mwenyekiti
wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki tarehe 30 Oktoba 1985 hadi
tarehe 24 Mei 1991 alipong'atuka kutoka madarakani.