2014-06-03 07:18:29

Balozi na mjenzi wa amani


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa vatican amemtaka Askofu mkuu Marek Zalewski, Balozi wa Vatican nchini Zimbabwe aliyewekwa wakfu kuwa Askofu hapo tarehe 31 Mei 2014 kuwa ni mjumbe wa umoja na mshikamano; balozi wa amani anapoendelea kumwakilisha Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbali mbali za dunia. Awe ni chombo cha majadiliano, haki na amani kati ya watu! Hizi ndizo sifa kuu ambazo Balozi wa Vatican anapaswa kuzionesha katika utekelezaji wa majukumu yake kwa niaba ya Baba Mtakatifu.

Askofu mkuu Marek Zalewski aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu na Balozi wa Zimbabwe kunako tarehe 25 Machi 2014. Ibada ya kumweka wakfu Askofu mkuu Zalewski imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali kutoka Poland.

Kardinali Parolin anasema kwamba, Ibada ya kumweka wakfu Askofu ndani ya Kanisa ni tukio muhimu sana kwani linamwezesha mhusika kupata neema ya kutakatifuza, kuongoza na kuwafundisha watu wa Mungu aliokabidhiwa kwake na Mama Kanisa kwa ajili ya kujenga na kuliimarisha Kanisa la Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake.

Hii ni neema ambayo inamwezesha Askofu kuwa kweli ni mhudumu wa Familia ya Mungu kwa kujisadaka zaidi kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili wote waweze kuguswa na harufu nzuri ya huduma ya upendo inayotolewa na Kristo pamoja na Kanisa lake. Askofu hana budi kuyajenga maisha yake katika Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Kwa Balozi wa Vatican anapaswa kuonesha kwamba, tofauti kati ya watu ni utajiri mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya huduma kwa Familia ya binadamu.

Balozi wa Vatican katika nchi yoyote ile ni daraja kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa Mahalia pamoja na Serikali, hii ndiyo huduma ambayo Askofu mkuu Zalewski anatumwa kuitekeleza nchini Zimbabwe kwa njia ya ushuhuda wa imani na maisha yake ya kila siku.

Askofu mkuu Zalewski tangu mwaka 1996 amefanya shughuli mbali mbali kwenye balozi za Vatican huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Umoja wa Mataifa, Uingereza, Ujerumani, Thailand, Singapore na Malaysia, hali inayoonesha kwamba, kweli ameiva katika majiundo yake, lakini haitoshi kuwa na mang'amuzi, masomo pamoja na uzoefu wa kazi. Kuna haja ya kujinyenyekesha mbele ya Kristo kwa njia ya sala ili kuonesha ujasiri wa Kristo mfufuka, kama walivyofanya wanafunzi wa Emmau. Kristo awe ni mwanga wa maisha na utume wake wa Kiaskofu.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anakumbusha kwamba, bado waamini na watu wenye mapenzi mema wanakumbuka tukio la kihistoria la kuwatangaza Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II. Poland imebahatika kulipatia Kanisa kiongozi shujaa mwenye ari na moyo wa kimissionari, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Poland imekuwa ni kisima cha watakatifu ndani ya Kanisa.

Askofu mkuu Marek Zalewski anatumwa na Mama Kanisa kutekeleza utume wake nchini Zimbabwe iliyojipatia uhuru wake kunako mwaka 1980 na kwa sasa inakabiliana na changamoto mbali mbali katika historia ya maisha yake. Ni Nchi ambayo ina waamini wa Kanisa Katoliki walio hai wanaotekeleza dhamana ya Uinjilishaji wa kina kwa njia ya huduma makini katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji. Hapa ndipo anapotumwa ili kuwa ni Balozi wa Vatican na mwakilishi maalum wa Baba Mtakatifu!







All the contents on this site are copyrighted ©.