2014-06-02 07:26:20

Upole, huruma na unyenyekevu!


Mpendwa msikilizaji wa Kanisa la Nyumbani, karibu kwa mara nyingine tena katika kipindi hiki. Kadiri ya desturi zetu Katoliki, mwezi huu wa sita tunauheshimu Moyo Mtakatifu wa Yesu. RealAudioMP3

Ni Kristo Yesu mwenyewe kwa uradhi wake, amedhihirisha siri ya moyo wake kwa nyakati mbalimbali, ambapo amewatokea watu wake aliowaridhia kama vile Mtakatifu Maria Margreth Alacoque. Ametaka moyo wake uliojitoa kwa ajili ya kutupenda sisi, UHESHIMIWE. Na kwa njia ya wachaji hao, Kristo Yesu ameonesha jinsi anavyoumizwa na kufuru zetu sisi wanadamu. Njia mmoja ya kuushukuru upendo wake mkuu, ni kuuheshimu moyo huo wa Yesu.

Moyo wa Yesu ni nini? Moyo Mtakatifu wa Yesu unamaanisha nafsi nzima ya Yesu mwenyewe, katika umungu na ubinadamu wake. Moyo huo unatafakariwa kwa tabia maalum ya upendo wake, huruma yake, unyenyekevu wake, upole wake, urafiki wake kwetu na maisha yake mazima ya ki-sadaka kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Ni moyo huo wa mapendo ndio uliojitoa sadaka kwa ajili yetu na sisi tunaomsadiki, tunaalikwa kumrudishia heshima, upendo, shukurani na ibada timilifu.

Kwa nini tuheshimu na kuabudu Moyo Mtakatifu wa Yesu?

Moyo wa Yesu ni Moyo wa Ki-Mungu ni Moyo wa Mungu. Moyo wa Yesu na upendo wake ni vitu muhimu vinavyounda Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Haviwezi kutenganishwa.


Kadiri ya Imani yetu Katoliki, Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya Sakramenti zote za Kanisa. Alipokuwa pale msalabani, askari mmoja wapo alimchoma ubavu kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji (Yoh. 19:34), na kutoka katika moyo huo wazi wa Mwokozi, ndipo lilizaliwa Kanisa, na zilizaliwa Sakramenti zote za Kanisa. Hivyo, kama Kanisa na Sakramenti zake vilizaliwa katika moyo wazi wa Mwokozi, basi Moyo huo ni kiini cha ibada zote katika Kanisa.


Tunauheshimu Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa sababu ni alama ya upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu. Moyo huo wa Yesu ndiyo uliodhihirisha pendo la Mungu kwetu sisi wanadamu. Moyo wa Yesu ni Nafsi nzima ya Kristo Yesu, inayofumbata pendo la Mungu kwetu sisi wanadamu.


Mwisho tunauheshimu moyo wa Yesu, kwa sababu Kristo Yesu, Bwana na mwokozi wa ulimwengu ametaka hivyo. Kristo anataka tuutazame moyo wake, tuchote neema katika chemchemi hiyo ya wokovu.

Kristo Mwenye amependa Upendo wa Moyo wake unaodhihirisha pendo la Baba, uwe pia mfano wa mapendo yetu. Anasema “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu” (Yoh. 15:9). Ni hamu kubwa ya Moyo wa Yesu uliotupenda, nasi tuishi katika mapendo yake. Ni kwa njia hiyo tutaweza kuhurumiana, kuinuana, kusaidiana, kuombeana na kupelekana kwa Mungu.

Swali linakuja, katika ulimwengu wetu huu uliofunikwa kwa blanketi zito la ubinafsi, uchoyo, wivu, kijicho, husuda, roho mbaya na kila aina ya mambo kama hayo, tutaishije Upendo wa Yesu? Katika ulimwengu huu ambapo leo wengi kwa matendo yetu tunaonekana ndio isharaza mwisho wa nyakati kama asemavyo Mtume Paulo “ Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao” (2Tim.3:1-5). Ndivyo wengi tulivyo. Tuuishije Upendo wa Yesu katika hali kama hiyo??

Yesu mwenyewe anatupatia mbinu za kuishi katika Pendo lake, anasema “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake” (Yoh. 15:10). Na anaendelea kusema “Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe. Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi” (Yoh 15:11-12).

Katika ibada zetu kwa Yesu, tunasali na kuomba tukisema, Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na moyo wako. Hiyo ndiyo iwe NIA na SALA ya kila mmoja wetu. Kwa mwezi huu na nyakati zote, dhamira hii iliongoze kanisa la nyumbani, yaani familia. Wanafamilia wakijaa upole na unyenyekevu, hapo wataweza kujenga amani. Familia nyingi zisizokuwa na tunu ya unyenyekevu, upendo hauna nafasi, amani haina nafasi; daima ni kelele, matusi, fujo na kila aina na madharau na manyanyaso.

Na kuna watu ni wakorofi hadi unajiuliza ‘hivi huyu ndugu ana moyo wa binadamu au moyo wa mbogo aliyekasirishwa’! Nyumbani- mkorofi, kazini- mkorofi, barabarani- mkorofi, kanisani- mkorofi, hata akiwa peke yake anajikorofisha tu, utashangaa anatukana tu peke yake na kugonga meza!! Dawa ni nini?? NI MOYO WA YESU TU!! Fadhila zake zitugeuze tuwe watu wema.

Tusipokuwa na fadhila za moyo wa Yesu, tunakuwa na tabia za kishetanishetani na hakika tunakuwa mizigo isiyobebeka kwa wengine. Kwa ukorofi wetu, wenzetu wanajuta na wanaumia sana kuishi na sisi. Baba wa familia kwa nini uwe mzigo kwa familia? Ukorofi utaacha lini? Mama, kwa nini uwe mzigo kwa familia? Watoto kwa nini muwe mizigo kwa wazazi na mtaani??

Sote tumgeukie Yesu SASA, tuombe fadhila za moyo wake zituelekee. Tuwe tayari kuongozwa na fadhila za Moyo wake kama tunavyozisali katika Litania ya Moyo Mtakatifu Wa Yesu. Nasi wanafamilia kwa roho ya umoja, kama tunapenda furaha, amani na mshikamano wa kifamilia, basi, na tusali pamoja tukisema EE YESU MWENYE MOYO MPOLE NA MNYENYEKEVU, FANYA MIOYO YETU IFANANE NA MOYO WAKO.
Kutoka katika Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.