Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 31 Mei 2014 amekutana na kuzungumza na kundi la watoto
kutoka Kusini mwa Italia lililofika mjini Roma kama sehemu ya majadiliano ya kidini
yanayoendeshwa na Baraza la Kipapa la utamaduni. Baba Mtakatifu amewashukuru watoto
hawa kwa kumpatia zawadi mbali mbali, ikiwa ni udongo kutoka kwenye Makatakombe ya
Mtakatifu Gennaro pamoja na mti wa mwanga ili kuifanya dunia kuwa ni mahali pazuri
zaidi pa kuishi. Amewakumbusha kwamba, Mtakatifu Gennaro ni kati ya watakatifu wanaoheshimiwa
sana mjini Napoli.
Udongo waliomletea Baba Mtakatifu uwasaidie kufukuza giza
katika maisha yao, tayari kuwa ni watoto wema wanaotembea katika mwanga wa maisha
mapya unaosheheni furaha na matumaini na kwamba jambo hili linawezekana kabisa. Baba
Mtakatifu Francisko katika mtindo wa mahojiano ya maswali na majibu aliwataka kujitahidi
kuondokana na chuki pamoja na uhasama wakijishikamanisha katika upendo kwa kusaidiana
na kutaabikiana kama ndugu wamoja, kwani Mungu ni upendo. Watoto hawana budi kutembea
katika mwanga wa upendo wakiwa na imani ya kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu.
Baba
Mtakatifu amewashukuru sana watoto hawa kwa kumtembelea na kwamba amefarijika sana.
Watoto kwa upande wao wanasema, wamefurahi kupindukia kuonana na kuzungumza na Baba
Mtakatifu Francisko. Mwishoni, amesali na kuwabariki ili kweli waweze kuwa ni vyombo
vya upendo katika hija ya maisha yao!