Chama cha Kitume cha Uamsho wa Kikatoliki, Jumapili tarehe 1 Juni 2014 kimewasha moto
wa Injili mjini Roma kuwashirikisha maelfu ya waamini kutoka ndani na nje ya Italia.
Limekuwa ni tukio la sala, tafakari na ushuhuda wa neema na baraka za Mungu kati ya
watu wake. Waamini wametumia nafasi hii pia kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani
zao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.
Kardinali Angelo Comastri amezungumzia
kuhusu umuhimu wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kama kielelezo cha ushuhuda
wa imani tendaji wakati huu Mama Kanisa anapojikita katika Uinjilishaji Mpya unaopaswa
kujielekeza zaidi katika maisha adili na manyofu. Padre Raniero Cantalamessa ametafakari
kuhusu umuhimu wa kumwamini Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu,
chemchemi na kiini cha imani ya Kanisa.
Wanachama wa Chama cha kitume cha Uamsho
wa Kikatoliki wamekumbushwa kwamba, wamempokea Roho Mtakatifu, ili awasaidie kuwa
kweli ni mashahidi waKristo hadi miisho ya dunia. Kumbe, changamoto ni kuendeleza
ujenzi wa ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Roho Mtakatifu
nikielelezo makini cha umoja na mshikamano wa dhati ndani ya Kanisa, kila mwamini
akijitahidi kutumia vyema karama na mapaji aliyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili
ya sita na utukufu wa Mungu.