2014-06-02 07:55:19

Jengeni utamaduni wa kuwakutanisha watu!


Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya vyombo vya upashanaji habari ni utamaduni unaoendelea kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya mwanadamu kwani kuna mambo mazuri ambayo yanapaswa kuendelezwa kwa ajili ya mafao ya wengi pamoja na kuangalia matatizo na changamoto zinazotolewa na vyombo hivi vya habari katika maisha ya mwanadamu.

Vyombo vya mawasiliano ya kijamii vinapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 48 ya Upashanaji habari Ulimwenguni iliyoadhimishwa tarehe 1 Juni 2014 wakati Mama Kanisa alipokuwa anasherehekea Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni.

Hivi ndivyo Baraza la Maaskofu katoliki Hispania linavyobainisha katika ujumbe wao kwa maadhimisho ya Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni. Kati ya changamoto kubwa zinazoendelea kujitokeza katika matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii ni baadhi ya watu kutengwa, na wengine kuendelea kuishi katika ulimwengu wa kufikirika, kiasi cha kushindwa kumwilisha upendo katika maisha yao ya kawaida. Kuna ombwe kubwa kati ya vijana wa kizazi kipya na wazazi wao.

Maaskofu wa Hispania wanakiri kwamba, kuna faida kubwa katika matumizi ya vyombo vya habari kwani watu waweza kupata habari nyingi kwa urahisi na wanaweza kubadilishana, kushirikishana mang’amuzi na kujenga umoja na mshikamano kati yao! Maaskofu wanaendelea kuwahimiza vijana kuhakikisha kwamba, wanajenga utamaduni wa kukutana, ili kweli teknolojia mpya iwe ni kwa ajili ya huduma kwa kwa binadamu na mafao ya wengi.

Wadau wa vyombo vya mawasiliano ya jamii wanayo dhamana kubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Kuna haja kwa jamii kuwa na majiundo makini ya matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, ili kuwa na ufahamu wa kina kuhusu jamii inayowazunguka na kufanya mang’amuzi ya kina ili kuchangia katika mchakato wa kueneza ukweli.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linabainisha kwamba, wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii wanafanya kazi katika mazingira magumu na yenye kinzani, wakati mwingine kwa ajili ya kutafuta mafao binafsi, kuliko hata kuzingatia ukweli, uzuri, wema na maadili, tunu msingi katika upashanaji habari. Uhuru, ukweli na maadili ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa badala ya kuendekeza umbea, uchochezi na kinzani za kijamii. Maaskofu wanawapongeza wadau mbali mbali wanaotekeleza majukumu yao katika vyombo vya upashanaji habari ulimwenguni!
All the contents on this site are copyrighted ©.