Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kinachoendelea kusababisha maafa makubwa nchini
Nigeria ni tatizo linalojikita katika masuala ya kijeshi, kiuchumi, kisiasa, kijamii
na hata kidini. Hivi ndivyo anavyobainisha Sultan Muhammad Sa’ad Abubakar III kutoka
Sokoto ambaye pia ni Rais wa Baraza kuu la Waislam nchini Nigeria wakati wa swala
ya kuombea wasichana waliotekwa nyara nchini Nigeria ili waweze kuachiliwa!
Anasema,
vitendo vya kigaidi havina nafasi katika dini ya Kiislam na kwamba, Waislam wote hawana
budi kuungana kwa pamoja kupinga vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia,
ili kuhakikisha kwamba, amani, utulivu na upendo vinatawala kati ya watu.
Kardinali
John Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria ameunga mkono tamko hili lililotolewa
na Sultan Muhammad Sa’aad Abubakar III kutoka Sokoto kwa kuonesha ujasiri na nia njema
kwa kile kinachoendelea kuzunguka katika mawazo na mioyo ya wananchi wengi nchini
Nigeria. Wasichana 250 waliotekwa ni tatizo kubwa, lakini linaloonesha hali tete ya
vitendo vya kigaidi ambavyo vimekuwa vikifanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram
nchini Nigeria.
Serikali ya Nigeria haina budi kulivalia njuga tatizo la Boko
Haram ili kung’oa mzizi wake kwa kuzingatia ukweli kwamba, kuna masuala ya kidini
yanayofumbatwa katika mashambulizi haya. Haitoshi kulaani vitendo vya kigaidi, lakini
kuna haja ya kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini yanayosimikwa katika ukweli,
uwazi na mafao ya wengi, ili kweli amani iweze kupatikana nchini Nigeria.