2014-06-02 07:34:06

Dhambi za vyombo vya habari!


Upotoshaji wa makusudi, umbea pamoja na kuwachafulia watu sifa njema ni kati ya dhambi kubwa zinazotendwa na vyom,bo vya upashanaji habari ulimwenguni na kusahau kwamba, vyombo hivi vina wajibu wa kutafuta ukweli, wema na uzuri mambo yanayopata chimbuko lake katika undani wa mwanadamu na asili yake ni Mungu mwenyewe! RealAudioMP3

Hii ndiyo kazi inayopaswa kutekelezwa na vyombo vya habari kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mwanadamu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanakimbia dhambi za vyombo vya habari!

Ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anazungumza na wajumbe wa Chama cha Corallo kinachoratibu matangazo yanayorushwa na vituo vya Radio na Televisheni zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki nchini Italia.

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe hawa kuwa na umoja katika shughuli zao. Huku wakisaidiana kama utekelezaji wa changamoto za kweli za Kiinjili katika hali ya unyenyekevu, kwa kutambua kwamba, kila mtu ana mchango wa pekee katika ustawi na maendeleo ya Kanisa. Tofauti za karama na vipaji ni utajiri mkubwa katika mkakati wa upashanaji habari!

Baba Mtakatifu aliwataka waamini walei kutambua nafasi na dhamana yao katika maisha na utume wa Kanisa pasi ya kuingilia mambo! Waamini walei watambue kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki: unabii, ukuhani na ufalme wa Kristo, dhamana wanayopaswa kuitekeleza kwa moyo wao wote. Mapadre wawaheshimu na kuwathamini waamini walei wanapotekeleza shughuli kadiri ya nafasi na utume wao! Sheria za Kanisa zisaidie kuweka amani na utulivu kati ya Makleri na Waamini walei kwa kujikita katika kuchuchumilia: ukweli, wema na uzuri.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, aliwataka wafanyakazi katika sekta ya upashanaji habari kujenga na kuimarisha urafiki wa kweli na wale wanaofanya nao kazi kwa kutambua kwamba, wao pia wanashiriki katika utume wa kuwavua watu kwa njia ya vyombo vyao vya upashanaji habari, kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, walipoitwa kwa mara ya kwanza.

Vyombo vya mawasiliano ya jamii viwasaidie watu kusikiliza sauti ya Kristo mchungaji mwema, katika hali ya amani na utulivu, ili kuwajengea watu matumaini pamoja na kuwa na uhakika wa maisha yao pasi na kukata tamaa! Kwa njia hii, vyombo vya upashanaji habari vinaweza kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa ufanisi mkubwa.

Baba Mtakatifu anawaalika wadau wa vyombo vya mawasiliano ya kijamii kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuwatangazia watu Injili ya Furaha, kwa kukazia mambo msingi yanayogusa maisha ya watu katika familia na jamii, kwa kuwajibika, daima wakiwa na lengo la kutafuta ukweli na kuwaheshimu watu wanaotazama au kusikiliza matangazo yao!

Baba Mtakatifu anasema, vyombo vya habari havina budi kujikita katika ubora unaozingatia kanuni maadili, utu wema pamoja na kutunza mazingira kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Kuwepo na muafaka katika matumizi ya maneno, ukimya na picha. Leo hii vyombo vya upashanaji habari vinachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, kiasi kwamba, mambo haya yamezoeleka na wala si tatizo tena! Hii ni hatari kubwa kwa afya za watu. Watu wajifunze kuheshimu na kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho na kimwili.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawahimiza wadau wa vyombo vya mawasiliano ya kijamii kuwa kweli ni Wasamaria wema kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wanaowahudumia, ili kwa njia ya huduma ya mawasiliano ya kijamii waweze kupata maisha bora zaidi; kwa kuwakirimia watu: imani, matumaini, furaha na mapendo!

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.