Kulikoni kusherekea msiba! Endapo unashindwa kuelewa na unashangaa juu ya sikukuu
ya kifo kadhalika ni vigumu sana kumfanyia sherehe mtu anayesafiri kwenda mbali mahali
atakakokaa kwa muda mrefu. Tunapoagana na wapendwa ndugu zetu tunasikitika na tunatulizana
kwa maneno kama haya: Kwa heri, Safari njema, Inshallah, Bye!
Somo la leo
ni aya za sura ya mwisho kabisa ya Injili ya Mateo. Sehemu hii yaweza kuwa ni ufupisho
wa historia ya maisha yote ya Yesu ambaye kwa muda mrefu aliishi Nazareti, baadaye
akafanya makazi huko Kafarnaumu pwani ya ziwa la Galilea, kisha alienda Yerusalemu
yalikomfika mauti na ndiyo ukawa mwisho wa habari. Tumekuja kutulizika pale Yesu alipofufuka.
Leo lakini anatuaga anaondoka, nasi tunasherekea na kuita sikukuu ya kupaa. Kulikoni
kumsherekea Yesu anayeondoka?
Sikukuu ya leo ambayo Yesu anaingia kwenye
ulimwengu wa Mungu na makao ya Baba, siyo safari ya kumpa “kwa heri” au “kwa heri
ya kuonana”. Safari hii ni ya “kuaga bila kuondoka.” Injili inaanza kwa kusema kwamba,
mitume kumi na mmoja walikusanyika kwenye mlima ambao walielekezwa kwenda. Mlima huo
ni ule wa heri nane. Hapa ndipo Yesu alipokutana mara ya kwanza na kikundi cha mitume.
Mahali hapo ndipo alianzia kufanya kazi.
Yesu kama binadamu alikuwa na
makazi yake Galilea na akitokea hapo aliweza kwenda sehemu mbalimbali kuhubiri. Pahala
hapo basi ni pa kuanzia na pa kuishia safari. Ni mwisho wa uwanja na mwanzo wa uwanja
mpya. Tungeweza pia kusema “Safari moja inaanzisha safari nyingine.” Kikundi kile
cha mitume kumi na mmoja, kimeagizwa na Yesu kukutanika hapo.
Yuda anakosekana.
Maelezo ya kukosekana Yuda aliyemsaliti Yesu yanaeleweka, lakini katika injili ya
leo huyu Yuda anatoa fundisho mpya. Yuda anasimama kama ishara au alama ya mtu anayefanya
mambo kinyume. Ni mtu asiyetaka kubadilika na anayeamua kufanya uchaguzi wake peke
yake. Ni mtu anayetumia uhuru kama anavyotaka yeye.
Kumbe yule asiyepanda
mlima ule wa Heri nane, hawezi kumwona Mfufuka, hawezi kupata mang’amuzi. Yuda ni
mfano halisi wa mtu huyo aliyejitenga, anayeamua kubaki kushabikia ulimwengu wa kale,
ulimwengu wa udanganyifu, ulimwengu wa biashara, ulimwengu wa kuuza na kununua, wa
kujadiliana juu ya bei ya bidhaa mbalimbali, ulimwengu wa kupiga siasa za kidunia
tu.
Hali halisi ya kikundi cha mitume kumi na mmoja ni tete, kimejaa mashaka,
woga, na mitume wanajisikia kama jeshi lililopigwa vibaya sana na kujeruhiwa, limesambaratishwa
na sasa linajaribu kujipanga upya. Kikundi hiki kinahitaji kutiwa nguvu ili kiweze
kuanza upya. Sasa kimekusanyika hapa mlimani. Mwinjili Matayo anasema: “Nao walipomwona
walimsujudia; lakini waliona shaka.” (28:17).
Neno hili “walipomwona”,
halimaanishi kule kuona kwa macho ya kimwili, bali ni kule kufaulu kuona hatima ya
yule aliyeweza kutoa maisha yake kwa ajili ya upendo. Kuona aina hiyo kunawezekana
tu kwa wale waliokwea mlima ule wa heri. Kumbe yabidi kwanza kuupanda mlimani huo,
halafu utaelewa kwamba hatima ya wale wanaopokea heri inayopendekezwa na mwalimu wao
ndiyo hatima ya maisha kamili katika Mungu kama ilivyotokea kwa Yesu wa Nazareti.
Yesu anapowajia mitume: “Wanamsujudia”: Huko kusujudia maana yake kuelewa
uwepo wa Mungu katika Yesu yaani kuionaa na kuipokea sura ya Mungu inayojionesha katika
Yesu, Mungu anayejitoa mwenyewe katika Upendo ndani ya Yesu. Yasemwa pia kwamba mitume
hawa “lakini waliona shaka.” Hapa unaona kwamba Kusujudia na Wasiwasi (woga) vinaenda
sambamba katika wanafunzi hawa.
Woga na wasiwasi vinakwenda pamoja na
imani. Huwezi kuepa wasiwasi. Hakutakuwa hata mara moja vithibiti vya imani, yaani
katika upendo hakuna hoja na vithibiti vya kiakili. Hiyo ni hali halisi kabisa ya
ubinadamu wetu. Ndiyo maana, Yesu hawagombezi na wala hajali tu, kwani anaona ni kitu
cha kawaida kwa wanafunzi. Hatuwezi kuwa na hoja na vithibiti vya ufufuko wa Yesu,
bali tunao uthibiti kutokana na mapendekezo aliyotuambia na kutufanyia Yesu mwenyewe
kutokana na maisha yake.
Yesu angewagombeza sana endapo wanafunzi wangekuwa
na uhakika kamili kabisa juu ya ufufuko, kwa sababu hatari kubwa ya kuwa na uhakika
katika imani mapato yake ni kuwa na masimamo mkali katika dini, na kuwalazimisha wote
kufuata itikadi za imani au dini yako.
Wanafunzi walikuwa na wasiwasi
kutokana na mapendekezo ya Yesu mwenyewe aliyoyatoa kabla juu ya mlima uleule waliokusanyika.
Wakizikumbuka zile heri nane wanaona zinakanganya na zinaletesha wasiwasi. Mathalani,
juu ya kuwa maskini, juu ya kuonewa, juu ya kudhulumiwa. Mashaka yanakuja zaidi pale
wanapojihoji na kujiuliza, “Hadi sasa tulikuwa tunamtegemea Yesu, kumbe sasa tumeishiana,
hivi tumepoteza kila kitu. Mambo yote mazuri aliyofundisha yamekuwa ndoto za bure.”
Yesu hatishiki, kwani anajua kwamba hawezi kuwa na hoja zinazoshikika mkononi kuhusu
mapendekezo aliyotoa.
Mfuasi wa Kristu anaweza kuwa katika kundi la akina
Yuda wasiotaka kubadili misimamo yao ya maisha na kumfuata Yesu. Lakini wale walio
katika imani na wanaomwabudu Yesu, hawatakosa kuwa na mashaka kama mitume. Kwa maana
hiyo, inabidi kila siku kuilisha imani yetu kwa Neno la Mungu. Tusipokuwa juu ya mlima
wa heri na badala yake tukashuka huko chini tutakuwa katika hali halisi ya maisha
ya ulimwengu, utaanza kuamini juu ya kile kinachooneka.
Yesu akawaambia:
“Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.” Katika vishawishi vyake kule jangwani
shetani alimpendekezea Yesu kuupata ulimwengu wote akimsujua. Ukifuata mantiki yake
angeweza kuuteka ulimwengu wote na kuutawala. Kumbe mamlaka hayo Yesu aliyakataa kwani
yeye alikuwa na mamlaka ya “mbinguni na duniani”. Nayo siyo mamlaka ya kutawala, bali
ni ya kutoa maisha na ya kuokoa.
Haya ndiyo mamlaka kwa ajili ya kuanza
upya maisha. Hivi anawaagiza “Enendeni” yaani kuanza safari ya kutembea. Kwa hiyo,
hatima ya injili ya Mateo ni mwanzo wa injili nyingine pamoja na Kristu mfufuka. Hatima
ya maisha ya Yesu siyo mwisho bali ni mwanzo. Kazi iliyoko ni “kuwafanya mataifa yote
kuwa wanafunzi.” Maana yake kuwafanya kuwa wasikilizaji, na wapokeao wa mapendekezo
haya ya Heri.
Haitoshi hiyo nadharia ya kufundisha wanafunzi, bali “Mkiwabatiza
kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Maana yake si kubatiza tu, bali ni
“kuzamisha” au “kujizamisha”, yaani kujizamisha au kujiingiza, kujitosa kabisa katika
maisha ya kimungu, ya Mungu Baba, ya Mungu Mwana na ya Mungu Roho Mtakatifu. Kazi
waliyokabidhiwa wafuasi inaendelea kwetu hata katika udhaifu wetu ni ile ya kuwazamisha
wengine na ya kujizamisha wenyewe katika maisha ya Mungu, maisha ya upendo. Kazi hiyo
amekabidhiwa kila mwamini.
Kisha inakuja sasa hatima nzuri tunayosherehekea
leo, kwamba “mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Kupaa si
kuachana na mfufuka, bali yuko pamoja nasi hata kama mahasa yetu hayawezi tena kumwona
na kumshika. Leo yuko nasi, yuko karibu zaidi nasi katika kazi yetu hii ya kujenga
ulimwengu katika maisha ya utatu na ya upendo. Kama hatima ya Yesu ni hiyo, basi tunayo
sababu ya kusherekea kupaa kwake, kwani amaeyapaisha maisha yetu juu mlimani. Tunaweza
pia kuusherekea msiba.
“Usihangaike usione hofu, yote yanapita Mungu hageuki,
utapata yote kwa saburi ukipenda kumshiriki Yeye, Mungu peke yake anatosha.”